Habari za Kitaifa

Hatimaye Kalonzo apewa nafasi ya kumwomboleza mgombea-mwenza wake Raila

Na CHARLES WASONGA October 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka alimsifia marehemu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga akiangazia safari yao ndefu ya kisiasa na kutotimia kwa ndoto yao na kuwafikisha Wakenya mahala ambapo aliita kama “canaan”.

Akiongea wakati wa ibada ya mazishi ya Raila Jumapili katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST), alisema Raila alikuwa rafiki wake wa karibu zaidi.

“Ningetaka kuongea na Raila moja kwa moja lakini sitapata nafasi hiyo tena. Kwa hakika historia yetu kisiasa ni ndefu zaidi ila hatukufaulu kushinda urais,” akasema.

Alisema kuwa katika uchaguzi mkuu wa 2017 wao kama wafuasi wa uliokuwa muungana wa NASA walimpa Raila jina la Joshua.

“Tulikuita Joshua. Lakini kwa bahati mbaya hatukufika Canaan,” akasema Bw Musyoka ambaye ni Makamu wa Rais wa zamani.

Kalonzo alikosa kuzungumza katika ibada ya kumuaga Raila mnamo Ijumaa jijini Nairobi, hali ambayo ilimkasirisha ikizingatiwa alikuwa mgombeaji mwenza wa Raila.