Helikopta iliyoanguka ilikuwa eneo ambako KDF inakarabati shule kufuatia agizo la Rais
NA CAROLINE WAFULA
TAIFA LEO sasa imebaini kwamba helikopta ya KDF iliyohusika kwenye mkasa iliondoka katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Cheptulel, Pokot Magharibi ambako kikosi cha jeshi kinakarabati shule hiyo iliyoharibiwa na majangili.
Hii inafuatia agizo la Rais William Ruto kwa jeshi wiki jana kukarabati shule zilizoathiriwa na ujangili katika eneo la Chesegon.
Bw Tito Lopuriang, mkazi ambaye alihudhuria mkutano huo wa maafisa wa jeshi anasema wanajeshi hao walikuwa wamemaliza kuhutubia umma katika shule hiyo kabla ya kuanza kuondoka kwa helikopta.
“Maafisa waliabiri ndege na baada ya muda mfupi tukaona moshi,” akasema.
Anasema kikosi cha usalama kikijumuisha KDF kilikuwa kimetembelea shule tano ambazo zimeathiriwa na ujangili kwa ajili ya kuzikarabati.
Alipokuwa anazindua kiwanda cha klinka ya saruji cha Cemtech katika eneo la Sebit, Pokot Magharibi Jumatatu wiki iliyopita, Rais Ruto alisema kwamba KDF watazuru eneo hilo katika muda wa siku mbili kuhakikisha shule zilizoharibiwa na wezi wa mifugo zimejengwa tena kwa ajili ya kufunguliwa kwa Muhula wa Pili.
“Haiwezekani kwamba katika karne ya 21, tuna watoto ambao hawaendi shule kwa sababu watu wachache wanasababisha utovu wa usalama,” akasema.
Rais alikuwa akimjibu Mbunge wa Sigor Peter Lochakapong ambaye alikuwa amelalamikia kufungwa kwa shule tano kwenye eneo bunge hilo na kwamba hazikuwa zimefunguliwa kwa muda wa miaka miwili kwa sababu ya ujangili na kumuomba kiongozi wa nchi atume jeshi kufanya ukarabati.