Helikopta sumbufu yahusishwa na ujangili, mashambulio Samburu
GEOFFREY ONDIEKI Na CHARLES WASONGA
HELIKOPTA moja ambayo hutua kila mara katika maeneo yanayozongwa na mashambulio ya majangili, inaendelea kuwatia wasiwasi wakazi wa Samburu Magharibi.
Wanasema mara ya mwisho kuiona hivi punde ilikuwa ni Jumamosi wiki jana.
Helikopta hiyo ambayo, hupaa karibu sana na ardhi, imehusishwa na mashambulio ya risasi ambayo yamechangia kuuawa kwa zaidi ya watu 80 katika eneo hilo tangu mwaka 2023.
Ufichuzi huo wa hivi karibuni umeashiria uwezekano wa wahalifu katika eneo hilo kusaidiwa na helikopta hiyo katika ushirikishwaji wa mashambulio yao.
Wakazi wametambua maeneo fulani katika eneobunge hilo ambako helikopta hiyo hutua yakiwemo maeneo ya bonde la Malaso, bonde la Kur Kur, Amaiya na sehemu za Pura.
Inasadifu kwamba maeneo hayo yameshuhudia mashambulio ya kila mara ya majangili waliojihami kwa silaha hatari.
Ni nyakati ambapo helikopta hiyo huonekana ambapo visa vya mashambulio huongezeka, hali inayowafanya wakazi kuihusisha na mashambulio hayo ya majangili.
Wakazi pia wanasema kuwa helikopta hiyo mara nyingi hutua katika maeneo fiche kama vile kwenye mitaro na mabonde ambako hukaa kwa muda kabla ya kupaa tena.
“Siku mbili baada ya helikopta hii kutua, huwa tunashambuliwa na majangili wenye bunduki. Serikali inayo habari kuhusu helikopta hii ila haijachukua hatua zozote,” akasema mzee wa eneo hilo Bw Samson Leparachao.
Kwa upande wake Bw Daniel Lesanjore, ambaye pia ni mkazi, anashuku operesheni ya helikopta hiyo.
“Mbona hutua katika mabonde pekee, mahala ambapo polisi hawawezi kufikia kwa urahisi?” akauliza Bw Lesanjore.
Minong’ono imeshamiri kuhusu umiliki wa helikopta hiyo kando na kushukiwa kuwa hutumiwa kusambaza silaha na mahitaji mengine ya kimsingi kwa majangili hao.
Wakazi sasa wanataka Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) kuingilia kati na kuanzisha upelelezi kubaini mmiliki wa helikopta hiyo na shughuli zake.
Mnamo Jumatano, diwani wa Wadi ya Loosuk Michael Lenamparasio aliitaka serikali itoe maelezo kuhusu suala hilo.
“Helikopta hiyo ingali inatua katika maeneo yanayozongwa na mashambulio ya majangili. Tunataka serikali ieleze ikiwa inayo ufahamu kuhusu helikopta hii,” diwani hiyo akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Mnamo Machi 2024, Mshirikishi wa Eneo la Bonde la Ufa Abdi Hassan alitoa amri kwa maafisa wa usalama waipige risasi helikopta yoyote itakayoonekana ikipaa katika maeneo yaliyozongwa na ujangili.
Lakini licha ya kutolewa kwa amri hiyo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.