Hizi barabara zitafungwa kwa muda, tafuta utakakopitia
MAMLAKA ya Barabara za Mijini (KURA). imetangaza kuwa itafunga kwa muda mfupi barabara 25 muhimu jijini Nairobi mnamo Desemba 1, 2024.
Katika notisi iliyotoa Novemba 27, mamlaka hiyo ilisema kwamba kufungwa kwa barabara hizo kunasababishwa na mbio za nusu marathoni za kuadhimisha Siku ya Ukimwi Duniani ambazo zitafanyika kati ya saa kumi na mbili na saa nne asubuhi.
Mbio hizo zinatarajiwa kuanza katika Uwanja wa Kitaifa wa Nyayo na kuendelea hadi Museum Hill kupitia Barabara Kuu ya Uhuru na Barabara ya Kenyatta, miongoni mwa barabara zingine ambazo shughuli zitatatizika kwa muda wa saa nne.
“Hii ni kuwaarifu madereva na umma kwa ujumla kwamba sehemu za barabara za Nairobi zitafungwa Jumapili Desemba 1 2024 kutoka kumi na mbili asubuhi hadi nne asubuhi kuwezesha nusu marathoni ya kuadhimisha siku ya Ukimwi Ulimwenguni,” ilisema sehemu ya ilani.
Barabara za Koinange, Muindi Mbingu, Wabera, Taifa, Harambee, Parliament na Haile Selassie pia zitaathirika.
Zingine ni Lower na Upper Hill, Mara, Ragat, Hospital na Elgon. Matumbato, Masaba, Wakihuri, Bunyala, Biashara, Enterprise, Dar es Salaam, Dunga, Lusaka na Aerodrome.
Mkurugenzi Mkuu wa KURA, Silas Kinoti, kwenye notisi hiyo pia aliomba radhi kwa usumbufu wowote na kuwataka Wakenya kujiandaa vilivyo na kutumia njia mbadala.
“Umma unaombwa kutumia njia mbadala kama utakavyoongozwa na trafiki na kujiandaa kwa usumbufu huu. Tunasikitika kwa usumbufu utakaosababishwa na tukio hili kwa utaratibu wako wa kawaida,” alisema.
Mbali na mbio hizi, kutakuwa na nyingine katika uwanja wa Nyayo, zikiwemo mbio za viti vya magurudumu za kilomita 10, mbio za kilomita 5 za familia pamoja na mbio za watoto.