Hofu IEBC butu inaweza kutumbukiza Kenya kwenye mzozo wa kikatiba
NA CHARLE WASONGA
TAIFA linakodolea macho mzozo mkubwa wa kikatiba kutokana ombwe uongozi uliopo katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Hii ni kutokana na hali kwamba nafasi ya mwenyekiti na zile za makamishna sita zingali wazi mwaka mmoja baada ya mwenyekiti wa zamani, Bw Wafula Chebukati na makamishna wawili kukamilisha muhula wao wa kuhudumu kutamatika Januari 17, 2023.
Nao wenzao wanne, Juliana Cherera (aliyekuwa Naibu Mwenyekiti), Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irene Masit walivuliwa nyadhifa zao Desemba 2022 kwa kupinga ushindi wa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, mwaka huo.
Kwa mujibu wa ushauri uliotolewa na Mwanasheria Mkuu Justin Muturi Oktoba 2023, IEBC haiwezi kuendesha chaguzi zozote wala kuchora upya mipaka ya maeneo wakilishi pasi na angalau makanimshna watatu afisini, kulingana na hitaji la kipengele cha 89 cha Katiba.
“Kipengele cha 89 cha Katiba, kinasema ni mwenyekiti na makamishna ndio huunda IEBC. Afisa Mkuu Mtendaji na maafisa wengine wa sekritariati ni wafanyakazi wa makamishna hawa. Kwa hivyo, ilivyo sasa ambapo hamna nafasi za mwenyekiti na makamishna ni wazi, asasi hiyo haina mamlaka kikatiba na kisheria kuendesha majukumu yake makuu ambayo ni; kuandaa chaguzi na kuchorwa upya mipaka ya maeneo wakilishi,” Bw Muturi akasema
“Bila makamishna, notisi za kuwezesha kufanyika kwa chaguzi zozote ndogo haziwezi kuchapishwa kwani kufanya hivyo kutakuwa ni kukiuka Katiba,” akaongeza.
Bw Muturi alitoa mwelekeo huo kutokana na kesi iliyowasilishwa mahakamani na wakili Brian Mbugua kwa niaba ya baadhi ya wakazi wa eneobunge la Banisa.
Wakazi hao, wapatao 100, waliitaka mahakama kuamuru kwamba sekritariati ya IEBC inayoongozwa na Afisa Mkuu Mtendaji Marjan Hussein Marjan iruhusiwe kuendesha uchaguzi mdogo katika eneobunge hilo.
Kiti cha ubunge cha Banisa, kilichoko Kaunti ya Garissa, kilisalia wazi baada ya kifo cha mbunge Hassan Maalin Hassan mnamo Mei 29, 2023.
Kiongozi huyo alikata roho akitibiwa katiika hospitali ya Mater, Nairobi baada ya kugongwa na mwendeshaji bodaboda akivuka barabara kuelekea katika msikiti mtaani South B, Nairobi.
Kando na hayo, IEBC ilivyo sasa haiwezi kuendesha shughuli ya uchoraji upya mipaka ya maeneobunge ilhali imesalia miezi miwili pekee kabla ya kutimu muda wa makataa ya kukamilishwa kwa zoezi hilo.
Kulingana na Katiba, shughuli hiyo inapasa kuendesha kati ya miaka minane na 12 baada ya mwaka wa mwisho tangu mipaka ilipochorwa mwisho.
Kwa kuwa mipaka ya sasa iliainishwa mara ya mwisho Machi 2012, ina maana kwamba IEBC inapasa iwe imekamilisha shughuli ya kuainishwa kwa mipaka kufikia Machi mwaka huu, 2024.
Wadadisi wa masuala ya siasa na sheria wanasema kuwa huenda Mkenya yeyote akawasilisha kesi kortini kuishtaki serikali kwa kukiuka kuvunja Katiba kwa msingi wa kufeli kuhakikisha kuwa “IEBC inatekeleza majukumu yake ya Kikatiba.”
“Ni kweli kwamba Kenya inaelekea kutumbukia katika mgogoro mkali wa kikatiba kutokana na hali kwamba IEBC haijawezeshwa kutekeleza majukumu yake. Kwa mfano kufikia sasa wakazi wa eneobunge la Banisa wamekaa kwa muda wa mwaka mmoja bila mbunge. Hii ni kinyume cha kipengele cha 94 kinachompa kila Mkenya haki ya kuwakilishwa bungeni,” anasema Wakili Aggrey Mwamu.
“Aidha, kufikia Machi mwaka huu IEBC inapasa kuwa imekamilisha shughuli ya uainishaji wa mipaka mipya ya maeneobunge na wadi. Bila makamishna afisini, ina maana kuwa shughuli hiyo imekwama,” anaongeza Bw Mwamu ambaye pia ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa.
Mtaalamu huyo anasema licha ya kwamba Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO) ilikubaliana kuhusu suala la uteuzi wa makamishna wapya, siasa za ubabe kati ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio ndio chimbuko la tatizo hili.