Yafichuka wafanyakazi 2,000 serikalini wana vyeti feki
NA CHARLES WASONGA
KUNA hofu kwamba huenda Wakenya wamekuwa wakihudumiwa na wahudumu feki katika hospitali kubwa za rufaa nchini, zikiwa ni pamoja na Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Moi (MTRH).
Hii ni kufuatia ufichuzi kwamba hospitali hizo mbili ni miongoni mwa asasi za umma ambako zaidi ya wahudumu 2,000 waliajiriwa kwa stakabadhi ghushi za masomo au taaluma.
Vyuo kadhaa vikuu vya umma pia ni miongoni mwa taasisi zenye wafanyakazi waliolaghai kwa kuwasilisha vyeti ghushi wakati wa kuajiriwa.
Kulingana na ripoti iliyotolewa na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) Jumanne, wizara za Usalama wa Ndani na Kawi pia zina idadi kubwa ya watumishi wenye vyeti feki vya masomo.
“Tunaamini kuwa takwimu za idadi hii sio mwisho kwani uchunguzi bado unaendelea na tunatarajia kupata visa vingi vya ulaghai wa aina hiyo,” Mwenyekiti wa PSC Anthony Muchiri akasema wakati wa kutolewa kwa ripoti katika makao makuu ya tume hiyo Nairobi.
Bw Muchiri alitaka hatua za haraka zichukuliwe kuzima uovu huo akitoa wito kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuwakamata wahusika.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak alisema tume yake itaanzisha mchakato wa kukomboa mishahara na marupurupu waliopokea wahudumu waliotumia vyeti feki vya masomo kupata nyadhifa wanazoshikilia katika utumishi wa umma.
Bw Muchiri alisema PSC ilianzisha uchunguzi kuhusu uovu huo mnamo Oktoba 2022, ambapo ililenga wizara kadha na mashirika ya serikali.
Kati ya visa 2,067 vilivyofichuliwa, idadi kubwa ni katika asasi kuu za serikali kuu.
Uchunguzi kuhusu uwepo wa uovu huo ulihusu ukaguzi wa rekodi za masomo za karibu miaka 10 iliyopita na uhakiki wa vyeti vya masomo uliofanywa kwa ushirikiano na asasi husika za kuendesha mitihani.
Ripoti hiyo inafichua mbinu kadha za kuendeleza uovu huo ikiwemo kubadilishwa kwa gredi wastani za KCSE, vyeti bandia vya KCSE na taarifa za uwongo za kufuzu.
PSC imependekeza kuwa visa hivyo vyote viwasilishwe kwa DCI na EACC ili wahusika washtakiwe
DCI pia itakomboa manufaa yoyote na mali iliyopatikana kwa njia hii ya ulaghai.
Isitoshe, wahusika watanyimwa manufaa mengine kama vile pensheni.