Habari za Kitaifa

Hofu Kioni ni ‘fuko’ ndani ya Upinzani

October 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KADRI siasa za kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 zinavyochacha, ndivyo upinzani nchini unavyokumbwa na misukosuko ya ndani, inayochochewa na kutoaminiana miongoni mwa viongozi wake.

Katikati ya mgogoro huo kuna Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Jeremiah Kioni, mwanasiasa aliyeongoza chama hicho cha aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta katika kipindi kigumu baada ya kustaafu, akipambana na makundi pinzani ndani ya chama kilichokuwa kikivutana kortini kuhusu uhalali wake.

Hata hivyo, kwa sasa, Bw Kioni anakabiliwa na madai yanayotishia mshikamano wa upinzani. Je, anasaidia kuimarisha muungano wa upinzani au anatekeleza ajenda fiche ya Uhuru ya kumsaidia aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kuwa mgombeaji wa urais wa upinzani dhidi ya Rais William Ruto mwaka 2027?

Baadhi ya viongozi wa upinzani sasa wanamchukulia Bw Kioni kama “kachero” ndani ya upinzani, hali inayofufua maswali kuhusu uaminifu wake, uongozi wake na mwelekeo halisi wa kile kinachoitwa ‘upinzani ulioungana’.

Wakati wa mazungumzo ya awali ya kuunda muungano wa upinzani, Bw Kioni alikuwa mwakilishi wa Jubilee mezani pamoja na viongozi kama Kalonzo Musyoka (Wiper), Eugene Wamalwa (DAP-K), Martha Karua (PLP), Justin Muturi (DP), na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.

Hata hivyo, miezi michache baadaye, Mwenyekiti wa Kitaifa wa Jubilee, Torome Saitoti, alionekana kuchukua nafasi ya Bw Kioni, ambaye alionekana kupotea kwenye shughuli za mazungumzo.

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari, Bw Gachagua na Musyoka walidaiwa kutoridhishwa na Bw Kioni, wakimshutumu kwa kuendesha ajenda ya upande mmoja, iliyompendelea Dkt Matiang’i.

Wapinzani wake wanasema Bw Kioni kwa kuwakashifu viongozi wenzake hadharani, na anayeonekana kuweka mbele zaidi chama cha Jubilee badala ya maslahi ya pamoja.

Jumanne iliyopita, Bw Kioni alimlaumu Bw Gachagua kwa madai ya kumshinikiza Dkt Matiang’i kujiondoa Jubilee wakati wa mazungumzo ya muungano na badala yake kuunga chama kidogo cha Kisii.

“Gachagua ni mradi wa Rais Ruto na anajaribu tu kuwapumbaza Wakenya,” alisema Kioni katika mahojiano hayo.

Kwa wengi ndani ya upinzani, Kioni anaonekana kuwa ‘mjumbe maalum’ wa Uhuru, akitafuta kuhakikisha Jubilee inakuwa chama kinachoweza kubadili mwelekeo wa muungano kwa masharti yake.

Msimamo wake huo umewakera hata viongozi wa chama cha DCP kinachohusishwa na Gachagua.

Naibu Kiongozi wa DCP, Cleophas Malala, alidai Jubilee imejificha kuendeleza ajenda ya chama tawala cha UDA, kinachoongozwa na Rais Ruto.

Katika mkutano wa DCP Kiambu wiki jana, Malala aliwaonya wafuasi wa upinzani kutohudhuria Kongamano Kuu la Jubilee (NDC) lililofanyika Ngong Racecourse Ijumaa.

“Hafla hiyo imelenga kudhoofisha ushawishi wa DCP na Gachagua katika Mlima Kenya. Msiwe sehemu ya kugawanya Mlima,” alionya Malala. Na kweli, kati ya viongozi wote wa upinzani, ni Dkt Matiang’i pekee aliyehudhuria NDC ya Jubilee.

Huku wenzake wakiongozwa na Gachagua wakihudhuria sherehe nyingine ya Martha Karua karibu na hapo.

Siku ya Jumatano, Mwenyekiti wa Jubilee, Bw Saitoti, alijitokeza kupunguza mvutano kwa kusema matamshi ya Kioni dhidi ya Gachagua yalikuwa ya kibinafsi na hayawakilishi msimamo wa chama.

“Chama kina vyombo rasmi vya kutoa kauli. Tulichoidhinisha kupitia NEC au NDC ndicho kinakuwa msimamo rasmi wa Jubilee,” alisema.

Katika mahojiano ya simu na Taifa Leo, Kioni alikiri kuwa yeye ni “mtumishi wa Uhuru” kwa kuwa ndiye Katibu Mkuu wa Jubilee, lakini alisisitiza kuwa anatafuta umoja wa upinzani, si mgawanyiko.

“Ninachoamini ni upinzani ulio imara na chama thabiti. Tunajenga Jubilee ili iwe na nguvu ya kuketi mezani kama mshirika sawa katika muungano,” alisema.

Kuhusu msimamo wake wa kumuunga Dkt Matiang’i, Kioni alisema kila chama kina haki ya kumsimamisha mgombeaji wake wa urais, lakini hatimaye vyama vitakubaliana kuhusu mgombea mmoja wa pamoja.

“Tutaweza kuwa na nguvu ikiwa kila chama ni thabiti. Tunaweza kuwa na wagombeaji tofauti lakini tukubaliane jinsi ya kupata mmoja,” alieleza.

Lakini kwa wengi ndani ya upinzani, jambo kuu si tu matamshi ya Kioni bali kivuli cha Uhuru.

Tangu kuondoka Ikulu mwaka 2022, Uhuru amekuwa kimya kisiasa, lakini ushawishi wake ndani ya Jubilee bado uko. Ni Uhuru aliyemlinda Kioni dhidi ya wapinzani waliotaka kumng’oa uongozi wa chama.

Hili limezua maswali: Je, Jubilee bado ni mshirika huru katika mazungumzo ya umoja wa upinzani au ni chombo cha kutekeleza ajenda ya rais wa zamani?

Mbunge wa Kathiani, Robert Mbui, mshirika wa Kalonzo, alisema haijulikani Jubilee inasimama wapi kisiasa kwa sasa.

“Wapo wanaoamini kuwa Kioni ni mwakilishi wa Uhuru, anayetaka kuhifadhi urithi wake kisiasa na kuwa na sauti kubwa katika maamuzi ya 2027,” alisema.

Profesa Gitile Naituli wa Chuo Kikuu cha Multi Media alionya kuwa vita vya maneno kati ya kambi ya Uhuru na Gachagua vinaweza kudhoofisha upinzani kuelekea 2027.

“Kambi ya Uhuru imeingiwa na hofu baada ya kutambua kuwa haina mvuto mkubwa Mlima Kenya. Kwa hivyo wanatafuta visingizio,” alisema Prof Naituli.