Hofu kuhusu Leba Dei Cotu ikichunguzwa
KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Kutetea Masilahi ya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli, leo ameitisha mkutano muhimu wa kukamilisha maandalizi ya sherehe za Leba Dei zitakazofanyika Jumatano wiki ijayo.
Bw Atwoli amechukua hatua hiyo kuzuia kutokea kwa changomoto kufuatia ukaguzi unaoendeshwa kuhusiana na matumizi ya fedha ya muungano.
Hii ni baada ya Mamlaka ya Kusimamia Walinzi wa Kibinafsi (PSRA) kuamuru kampuni zote za kutoa huduma za ulinzi wa kibinafsi kuwasilisha katika kipindi cha siku tatu zijazo, maelezo kuhusu makato ya ada za vyama vya wafanyakazi kutoka kwa mishahara ya walinzi wao ambayo yaliwasilishwa kwa Cotu ndani ya miezi 36 iliyopita.
Aidha, PSRA inazitaka kampuni hizo kuwasilisha taarifa zote za kifedha zilizotuma kwa Cotu kuhusu makato ya ada za makato hayo na jinsi zilivyowasilishwa kwa muungano huo wa vyama vya wafanyakazi.
Haya yanajiri wakati ambapo mamlaka hiyo inaendesha ukaguzi kuhusu ukusanyaji na matumizi ya pesa zote ambazo zimekatwa kutoka kwa angalau walinzi milioni 1.3 wa kibinafsi na kuwasilishwa kwa Cotu, na kampuni husika, ndani ya miaka mitatu iliyopita.
Afisa Mkuu Mtendaji wa PSRA, Fazul Mohamed, katika barua alizoziandikia kampuni hizo, na Taifa Leo ikapata nakala zake jana, anasema kundi la wakaguzi kutoka mamlaka hiyo wakiongozwa na Philip Okello na Clinton Ingalula wanasimamia mchakato huo wa ukaguzi.
Makala ya 59
“Zingatia kuwa usipotekeleza agizo hili usajili na leseni yake itafutiliwa mbali kulingana na Sehemu ya 32 ya Kanuni kuhusu Ulinzi wa Kibinafsi Nambari 13 ya 2016,” ikasema sehemu ya barua ya Bw Mohamed kwa kampuni hizo.
Duru zinasema kuwa mvutano kati ya Cotu na PSRA inatisha kuvuruga mipango ya maandalizi ya makala ya 59 ya sherehe la Leba Dei mnamo Mei 1, 2024.
Hii ni kwa sababu walinzi wa kibinafsi ni miongoni mwa wahusika wakuu katika sherehe hizo ambazo huandaliwa kwa pamoja na Cotu na serikali kupitia Wizara ya Leba.
Taifa Leo imefahamishwa kwamba leo Bw Atwoli ataongoza mkutano wa mwisho wa Kamati ya Siku Kuu ya Kimataifa ya Leba Deo katika makao makuu ya Cotu, Jumba la Solidarity, Nairobi kuanzia saa nne asubuhi.
Ada za vyama
Kamati hiyo inashirikisha Joel Chebii (Mwenyekiti), Benson Okwaro (Naibu Katibu Mkuu), Rebecca Nyathogora (Mweka Hazina ), Wycliffe Nyamwatta, Ernest Nadome, Nelson Mwaniki, Albert Njeru, Boniface Kavuvi, Isaac Andabwa, Rose Omamo, Teresia Njeri, Moss Ndiema na Julius Maina.
Wiki iliyopita, Bw Atwoli aliishambulia vikali mamlaka ya PSRA kuhusiana na agizo lake kwamba kampuni za ulinzi wa kibinafsi zikome kukata na kuwasilisha kwa Cotu ada za vyama vya wafanyakazi wao.
Bw Atwoli alimsuta Bw Mohamed kwa “kuvuruga na kuingilia shughuli za Chama cha Kitaifa cha Kutetea Masilahi Walinzi wa Kibinafsi na washirika wake kama vile Wizara ya Leba, Shirikisho la Waajiri Nchini (FKE) na Cotu.