Habari za Kitaifa

Hofu watoto 8,000 wakipachikwa mimba Kajiado

November 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAJIADO ni miongoni mwa kaunti ambazo zimesajili idadi ya kutisha ya mimba za utotoni huku visa 8,000 vikiripotiwa katika kipindi cha miaka mitano.

Kulingana na Mshirikishi wa Idara ya Afya ya Kaunti ya Kajiado, Bi Karen Kamau, ni wasichana 1,783 pekee kati ya wasichana wajawazito wenye umri wa kati ya miaka 15-18 na wasichana 947 wenye umri kati ya miaka 10-14 walitafuta huduma za afya katika vituo vya afya kati ya 2023- 2024.

Wengine walijifungua kwa usaidizi wa wakunga nyumbani na kuzidi kuhatarisha maisha yao.

Haya yamefichuliwa katika takwimu kutoka vituo mbalimbali vya afya katika kaunti hiyo.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango wa “She Rise” uliofanyika Kajiado mnamo Jumatatu, ambao pia ulitumiwa kuzindua Siku 16 za kupinga Dhuluma za Jinsia, wadau mbalimbali walieleza wasiwasi kuhusu kuibuka kwa akina mama wachanga wanaoishi katika umaskini uliokithiri na kukabiliwa na unyanyapaa kutoka kwa jamii.

“Mimba za watoto katika kaunti ya Kajiado hushinda aina nyingine yoyote ya Unyanyasaji wa Kingono na Kijinsia (SGBV) unaotokana na mila potovu ikiwa ni pamoja na ukeketaji na ndoa za utotoni zinazoathiri elimu rasmi,” Bi Kamau alisema.

Aliongeza kuwa hii ni licha ya mimba za utotoni kupungua katika kipindi cha miaka mitano iliyopita kutoka asilimia 21 hadi asilimia 18.3.

“Takwimu zinabaki kuwa za kutisha. Mimba nyingi za watoto huishia kutoripotiwa huku wasichana wengi wakihudumiwa na wakunga wa jadi maeneo ya vijijini,” aliongeza.

Mpango wa ‘She Rise’ ni wa miezi 18 chini ya muungano wa mashirika mbalimbali yasiyo ya kiserikali kwa ushirikiano na ngazi mbili za serikali na unalenga kuwapa kina mama wachanga nafasi ya kupata mafunzo ya ufundi bure kama njia ya kuwawezesha kiuchumi.

Watekelezaji wa mpango huu wamepokea maombi yasiyopungua 500 kutoka kwa akina mama wachanga ambao wangependa kurejea shuleni baada ya kujifungua.

“Kwa sasa tunaweza kuchukua wasichana 30 pekee” alisema mkurugenzi wa ‘She Rise’, Bi Jedidiah Lemaron.

Bi Cicilia Nashipae, 19, ambaye alijifungua miaka mitatu iliyopita akiwa bado shuleni, alisema wenzake wanapitia changamoto nyingi kijijini baada ya kuacha shule.

“Kwa kawaida tunakejeliwa na kulaaniwa na jamii lakini tunaamini tunayo nafasi ya kubadilisha maisha yetu na kutimiza ndoto zetu.

Mkurugenzi wa bodi ya kupinga ukeketaji Bi Benedetta Loloju, alisema visa vya ukeketaji na mimba za utotoni vinatatiza wasichana wengi katika Kaunti ya Kajiado hasa katika maeneo ya mashambani.

“Visa vimepungua ingawa kwa asilimia ndogo. Tatizo hili linahitaji mbinu kamili ili kuwawezesha wasichana kiuchumi. Tunataka kuhakikisha kila msichana anapata kozi ya kujitegemea. Mtoto sio laana, tunataka kubadilisha hali sasa,” alisema Bi Loloju.