Habari za Kitaifa

Hofu ya maandamano ya Nane Nane yafunga maduka jijini Nairobi polisi wakishika doria

Na BENSON MATHEKA August 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

POLISI nchini Kenya wameimarisha usalama Nairobi kwa kuweka vizuizi kwenye barabara kuu za kuingia jijini huku maduka mengi yakifungwa kwa hofu ya  maandamano mapya ya kupinga serikali yaliyopangwa kufanyika Alhamisi.

Polisi walimwagwa katikati ya jiji na kuna vizuizi katika barabara za Waiyaki, Thika na Mombasa.

Magari ni machache katikati ya jiji huku biashara nyingi zikifungwa.

Kwa miezi miwili sasa, Kenya imekumbwa na maandamano yakiongozwa na vijana wanaopinga utawala wa Rais William Ruto  ambaye amekuwa mamlakani kwa karibu miaka miwili.

Kaimu mkuu wa polisi Gilbert Masengeli  ametoa onyo kali kwa “wahalifu” wanaonuia kutumia  maandamano hayo kupora na kuharibu mali.

Ameonya waandamanaji kuepuka  “maeneo yaliyolindwa” kama vile uwanja wa ndege wa kimataifa na Ikulu; makazi rasmi ya rais.

Katika chapisho kwenye X, Kaimu Inspekta wa Polisi Masengeli alisema maafisa wa usalama wa  kutosha wametumwa  jijini kudumisha usalama, lakini akashauri umma “kuchukua tahadhari zaidi wakiwa katika maeneo yenye msongamano wa watu ambayo huenda yakakumbwa na ghasia.

Katika taarifa yake Jumatano, Masengeli alionya kuhusu wahalifu wanaopanga kutumia Maandamano ya Nane Nane kutekeleza uhalifu.

Takriban watu 60 wameuawa tangu maandamano hayo yaanze. Yalianza kuelezea pingamizi za vijana dhidi ya mapendekezo ya nyongeza ya ushuru lakini sasa yamechukua mkondo tofauti vijana wakielezea kutoridhishwa kwao na matumizi mabaya ya rasilmali za umma na kero ya ufisadi.