Huenda ukalipa karo zaidi kuliko inavyofaa
NA WANDERI KAMAU
WAZAZI nchini wanakabiliwa na kibarua kigumu kuanzia Jumatatu, wanapojitayarisha kugharimia mahitaji ya wana wao wanaorejea shuleni, baada ya kukaa nao kipindi cha likizo ya Krismasi na Mwaka Mpya.
Baadhi ya gharama zinzowaandama wazazi wengi ni kiwango cha juu cha karo, kwani baadhi ya shule nchini tayari zimetangaza kuongeza karo zinazowatoza wanafunzi wake.
Uchunguzi wa Taifa Jumapili katika maeneo tofauti nchini, umebaini kwamba huenda wazazi wengi wakashindwa kuwalipia wana wao karo hizo, hasa baada ya wengi wao kutumia pesa nyingi kwa familia zao kwenye likizo ya Desemba.
Kwa mfano, katika Shule ya Kitaifa ya Mang’u, iliyo katika Kaunti ya Kiambu, mzazi atalazimika kumlipia mwanawe karo ya jumla ya Sh91,000 kwa mwaka.
Hii ni baada ya kuondoa Sh22,000 zinazotolewa na serikali kama msaada kwa wanafunzi walio katika shule za upili. Hivyo, hilo linamaanisha kuwa kijumla, karo ya mwanafunzi mmoja katika shule hiyo ni Sh113,150!
Wazazi kadhaa tuliozungumza nao kutoka shule hiyo walisema itakuwa vigumu kumudu kiwango hicho cha juu cha karo, kutokana na gharama ya juu ya maisha.
“Huu ni mtihani mkubwa na mgumu sana kwetu. Mwaka 2023, karo ya mwaka mmoja ilikuwa Sh80,000 kiwastani, ukijumuisha fedha zinazotolewa na serikali kama msaada kwa mwanafunzi,” akasema mzazi ambaye hakutaka kutajwa.
Katika Shule ya Wanaoishi na Ulemavu ya Kairuni, iliyo katika eneo la Chogoria, Kaunti ya Meru, mhisani anayemfadhili mwanafunzi mmoja alilazimika kuomba usaidizi kwenye mitandao ya kijamii, kwani mwanafunzi huyo hawezi kumudu karo ya juu inayotozwa na shule hiyo.
Kulingana na Bi Wanja Mwaura, anayemfadhili mwanafunzi huyo, ana deni la Sh25,000 huku akitarajiwa kulipa karo nyingine ya Sh27,000 mwaka 2024.
“Kutokana na hali hii, ninaomba wahisani kujitokeza kunisaidia kuchangisha Sh52,000 kumwezesha mwanafunzi huyo kurejea shuleni,” akasema Bi Mwaura.
Hata hivyo, mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA), Bw Silas Obuhatsa, alisema kuwa bado hawajapokea malalamishi yoyote au visa ambapo shule zimeongeza karo ya wanafunzi bila kuzingatia taratibu zilizowekwa na Wizara ya Elimu.
“Kama chama, bado hatujaokea malalamishi yoyote. Hata hivyo, hilo halimaanishi kwamba tutakuwa kimya ikiwa mtindo huo utakuwa ukiendelea. Tutaishtaki shule ama mwalimu mkuu yeyote atakayewaongezea karo wazazi bila idhini kutoka kwa Wizara ya Elimu,” akasema mwenyekiti huyo kwenye mahojiano na Taifa Jumapili mnamo Jumamosi.
Kando na ugumu wa kulipa karo, wazazi pia wanakabiliwa na gharama kubwa ya kuwanunulia wanao bidhaa za matumizi ya msingi, hasa wale wanaojiunga na Kidato cha Kwanza na Sekondari ya Msingi (JSS).
Kwenye mahojiano jana, Bi Mary Wangui, ambaye ni mkazi wa Kaunti ya Nakuru, alisema ametumia zaidi ya Sh20,000 kununua bidhaa za matumizi za mwanawe, anayetarajia kujiunga na Shule ya Upili ya Wasichana ya Wanjohi, iliyo katika Kaunti ya Nyandarua.
“Nikikadiria pesa nilizotumia kumnunulia sare za shule, sanduku, vitabu vinavyohitajika, sare maalum za michezo kati ya nyingine, hazijapungua Sh20,000. Ni mzigo mzito kwa wazazi wengi,” akasema.
Kero nyingine inayowaandama wazazi wanaotarajia kuwapeleka wanao katika JSS ni tishio la walimu walioajiriwa kwa mfumo wa kandarasi na serikali katika shule hizo kugoma.
Wiki iliyopita, walimu hao walitishia kugoma kuanzia kesho, ikiwa serikali haitawaajiri wa mfumo wa kudumu.
“Mkataba wa walimu hao unakamilika mwezi ujao. Tumepata ripoti kwamba kuna mpango wa kuwaongezea mkataba huo kwa mwaka mmoja zaidi. Hatutakubali hivyo. Ni lazima walimu hao waajiriwe kwa mfumo wa kudumu na Tume ya Kuwaajiri Walimu (TSC),” akasema Bw Zablon Awange, aliye Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Sekondari na Vyuo Anuwai Kenya (Kuppet).
Licha ya tishio hizo, serikali haijatoa taarifa yoyote.