Habari za Kitaifa

Hutaweza kununua ‘tokens’ kwa siku mbili – KPLC

May 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA KEVIN CHERUIYOT

KAMPUNI ya Kenya Power (KPLC) imetangaza kuwa wateja hawataweza kulipia au kununua umeme pamoja na kupokea huduma nyingine kuanzia Jumapili hii hadi Jumatatu ijayo.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, watakuwa wakiboresha mitambo yao ili kuimarisha huduma zao kwa wateja katika kipindi hicho.

Kupitia notisi iliyotumwa mnamo Jumatatu, KPLC ilisema wateja watakaolipia umeme siku hizo hawatafanikiwa kutokana na maboresho ya mitambo yatakayokuwa yakiendelea.

“Hakutakuwa na huduma za kununua umeme kuanzia Jumapili, Juni 2 saa nne usiku hadi saa nne Juni 3. Wakati huo tutakuwa tukifanyia ukarabati mitambo yetu,” ikasema taarifa kutoka KPLC.

Wateja wanaolipia umeme na kupata tokeni hutumia mfumo wa bili ya M-Pesa Nambari 888880, Airtel Money na kupitia benki mbalimbali.

“Tunawaomba wateja wetu wanunue umeme kabla ya siku hizo mbili ili kuzuia kutatizika,” ikaongeza taarifa hiyo.

Februari, wateja walilemewa kununua umeme kutokana na tatizo la mitambo ambalo lilirekebishwa baadaye.

“Kufuatia hitilafu ambayo ilitokea juzi na kusababisha mchakato wa kulipia umeme kutatizika, tungependa kuwaambia wateja wetu kuwa tulisuluhisha changamoto hiyo Jumatatu. Sasa wateja wanaweza kununua umeme kupitia nambari ya M-Pesa 888880,” ikasema notisi hiyo.

Huku KPLC ikilenga kupambana na wizi wa umeme, Rais William Ruto hivi majuzi aliamrisha kampuni hiyo isiwakatie wale ambao wameunganisha umeme kiharamu bali iwawekee mita ambapo matumizi yao yatafuatiliwa na watachangia ushuru.

Wizi wa umeme hasa umekithiri katika mitaa ya mabanda. Pia jana, mkataba wa kuunganisha maeneo yote na umeme ulitiwa saini katika ikulu ya Nairobi, hafla ambayo iliongozwa na Rais Ruto na Waziri wa Kawi Davis Chirchir.

Mapema mwaka huu, Rais Ruto alisema serikali yake ilikuwa imetenga Sh49 bilioni kusaidia katika mradi huo wa kuunganisha umeme maeneo yote nchini.

Mradi huo ulianzishwa katika utawala uliopita wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.