Huzuni mbunge akiuawa kwa kupigwa risasi
MSIBA umekumba asasi ya bunge kwa mara nyingine kufuatia kifo cha ghafla cha mbunge wa Kasipul Charles Ong’ondo Were.
Mbunge huyo wa chama cha ODM alishambuliwa kwa risasi na wahuni mnamo Jumatano jioni, Aprili 30, 2025, katika barabara ya Ngong, karibu na mzunguko wa Hifadhi ya Maiti ya City, Nairobi na watu wawili waliokuwa wakisafiri kwa piki piki.
Akithibitisha kisa hicho Kamanda wa Polisi katika Kaunti ya Nairobi George Seda alisema kiini cha mauaji ya mbunge huyo hakikujulikana mara moja.
“Ripoti za ambazo tulipokea awali ni kwamba Mheshimiwa aliuawa na watu wawili wenye bunduki walioshambulia gari lake katika barabara ya Ngong’ karibu na Hifadhi ya City. Hata hivyo, kufikia sasa hatujabaini kilichosababisha mauaji hayo. Tumeanzisha uchunguzi huku tukisaka wahalifu hao,” Bw Seda akaambia wanahabari Nairobi Hospital ambako mbunge huyo alikimbizwa kabla ya kukata roho.
Bw Were alikimbizwa hospitalini na dereva wake ambaye alisazwa katika shambulio hilo ambalo limewaacha wabunge na Wakenya kwa mshangao.
Duru zinasema kuwa wavamizi hao walikuwa wakimfuata Mbunge huyo kutoka majengo ya Bunge na walimshambulia Ngong Road, eneo ambalo hushuhudia msongamano wa magari nyakati za jioni haswa siku za kazi, Jumatatu hadi Ijumaa.
Inasemekana kuwa walivunja kioo cha gari lake kwa kifaa butu kabla ya kummiminia risasi kwa karibu.
Bw Were, ambaye wabunge wenzake humtambua kama “Sir Charles” anahudumu muhula wa pili baada ya kuchaguliwa kwa mara ya kwanza katika uchaguzi mkuu wa 2017 kwa tiketi ya ODM.
Katika Bunge la 13, alikuwa akihudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa Kuhusu Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kanda, wadhifa ambao alitunukiwa mwezi Machi mwaka huu, 2025, kutokana na uaminifu kwa serikali jumuishi.
Aidha, Mbunge huyo wa Kasipul alikuwa mwanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uchumi wa Majini na Unyunyiziaji.
Kabla ya kuchaguliwa kama Mbunge alikuwa mfanyabiashara mashuhuri mjini Meru.
Kifo cha Bw Were kimejiri mwezi mmoja baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Malava Malulu Injendi na aliyekuwa Seneta wa Baringo William Cheptumo.
Wabunge wengi walishangazwa na kifo cha ghafla cha mwenzao waliyemtaja kama kiongozi mchapakazi na aliyechangia pakubwa katika shughuli za maendeleo katika eneobunge lake lililoko Kaunti ya Homa Bay.