Huzuni Mwanahabari maarufu wa NTV, Rita Tinina akiaga dunia
NA WANDERI KAMAU
MWANAHABARI maarufu wa kituo cha televisheni cha NTV, Rita Tinina, ameaga dunia.
Kituo hicho kinamilikiwa na shirika la habari la Nation Media Group (NMG).
Mwili wa mwanahabari huyo ulipatikana nyumbani kwake katika eneo la Kileleshwa, jijini Nairobi, Jumapili, Machi 17, 2024.
Hata hivyo, hakukuwa na thibitisho lolote maalum kuhusu kiini cha kifo chake.
Mkurugenzi Mkuu wa Uhariri katika shirika hilo, Bw Joe Ageyo, alithibitisha kifo chake.
“Asubuhi ya leo (Jumapili), tulipokea habari za kusikitisha kuwa mwenzetu Rita Tinina alikuwa ameaga dunia katika nyumba yake. Alikuwa ametarajiwa kuwa kazini leo japo hakufika. Familia imeomba kupewa nafasi kumwomboleza mpendwa wao katika wakati huu mgumu. Nawaomba nyote muwe watulivu tunapongoja maelezo zaidi kuhusu habari hizi za kuhuzunisha,” akasema Bw Ageyo kwenye taarifa.
Polisi walisema kuwa mjakazi wake alijawa na hofu wakati mwanahabari huyo alikosa kuamka mwendo wa saa nne asubuhi, hali iliyomfanya kuwapigia simu marafiki wake.
Polisi walisema kuwa mtoto wake wa miaka saba aliyemwambia mjakazi huyo kwamba mamake alionekana kupoteza fahamu.
Mwili wake ulipelekwa katika mochari ya Umash, Nairobi.
Marehemu amekuwa kwenye tasnia ya uanahabari kwa zaidi ya miongo miwili.
Mwnzoni, alihudumu kama ripota katika NTV, ambapo baadaye alijiunga na kituo cha televisheni cha KTN.
Alijiunga tena na NTV Oktoba mwaka uliopita, 2023.