Habari za Kitaifa

Huzuni tineja akitoweka ghafla kutoka kanisani

Na STANLEY NGOTHO August 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

BI Mary Wanjiku Njoroge aliachwa na majonzi Jumamosi Agosti 17, 2014 baada ya mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka 16 kutoweka alipokuwa akihudhuria semina ya vijana katika kanisa moja. 

Siku hiyo mvulana huyo kwa jina Samuel Kamau aliyeandamana na dadake mkubwa Grace Gathoni, aliondoka nyumbani kwao Kitengela saa moja na nusu asubuhi na kuelekea katika Kanisa la Kenya Assemblies of God (KAG), tawi la Kitengela New Valley Road.

Wawili hao walitarajia kukutana na wenzao katika uwanja mdogo kanisani ili kuabiri gari la kanisa hili kuelekea semina hiyo katika KAG, tawi la Athi River, katika kaunti jirani ya Machakos.

Lakini tineja huyo alitoweka dakika 30 baada ya yeye na dadake mkubwa kuwasili katika kanisa hilo.

Taifa Leo ilipokutana na familia hiyo nyumbani kwao katika eneo la Kitengela Sixers Jumamosi, Bi Njoroge na bintiye Grace Gathoni walionekana kujawa na huzuni kufuatia kutoweka kwa Kamau.

Bi Gathoni, 20, aliambia Taifa Leo kwamba walitembea kwa miguu mwendo wa kilomita tatu hadi kanisa hilo, KAG, Kitengela.

Wakiwa njiani, alikuwa akicheza kwa simu yake.

“Tulipofika kanisani tuliamua kusubiri wengine ili kuanze safari kwa pamoja kuelekea Athi River kwa semina hiyo,” akasema.

Bi Gathoni alisema mwendo wa saa mbili na nusu asubuhi, alijitenga na wenzake na kuingia chooni hatua chache kutoka kwa jengo la kanisa.

“Lakini niliporejea dakika chache baadaye kakangu, Kamau, hakuwepo. Alikuwa amemwachia simu yake ambayo alikuwa akitumia kucheza michezo ya mitandaoni,” akaeleza.

“Nilishtuka baada ya kumkosa mahalI ambako nilimwacha. Nilianza kumtafuta lakini sikumpata. Mtu fulani alisema alimwona akiondoka kupitia lango la kanisa kabla ya kutoweka kabisa,” Bw Gathoni akaeleza huku machozi yakimtoka.