Ichung’wah amwaga Sh138 milioni kujiweka pazuri kwa dili ya Affordable Housing
KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah amenunua hisa katika kampuni ya mikopo ya ujenzi wa nyumba, Housing Finance Group (HF), akitarajia kuchuma katika sekta ya nyumba yenye utajiri mkubwa.
Duru katika asasi ya kusimamia biashara ya hisa zimefichua kuwa mbunge huyo wa Kikuyu alinunua hisa milioni 18 za thamani ya Sh138.3 milioni katika soko huru.
Hatua hii inamfanya Bw Ichung’wah kuwa mmiliki wa asilimia moja ya hisa katika kampuni hiyo ya kutoa ufadhili katika sekta ya nyumba.
Mbunge huyo alijitetea akisema kuwa alichukua mkopo kununua hisa hizo za HF, zenye uwezo wa kuzaa faida kubwa kwani kampuni hiyo pia inashiriki katika biashara ya benki.
“Nilivutiwa na kampuni ya HF kwa sababu imeimarika kutoka ilivyokuwa ikirekodi hasara hadi hali yake ya sasa ambapo inaandikisha faida kutokana na usimamizi mzuri,” Bw Ichung’wah akasema kwenye mahojiano.
“Zamani ilijihusisha na ujenzi wa nyumba, shughuli ambayo faida yake ni ndogo, lakini sasa imekumbatia biashara ya benki inayoleta faida ya haraka,” akaongeza.
Hatua ya Bw Ichung’wah kujiunga kwenye orodha ya wenyehisa wa kampuni ya HF inafuatia ile ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Ushuru (KRA), Antony Mwaura.
Bw Mwaura pamoja na mkewe na bintiye wanamiliki asilimia 12.72 ya hisa katika HF, kitengo cha benki.
Hisa hizo ni za thamani ya Sh1.6 bilioni.
Familia ya Bw Mwaura, ambaye sasa ni mwenyekiti wa Mamlaka ya Kusimamia Barabara za Mashambani (KeRRA) ndiyo ya pili kwa hisa nyingi katika HF nyuma ya kampuni ya Britam Holding inayomiliki asilimia 48.17 ya hisa.
Bw Ichung’wah na Mwaura ni wandani wa karibu wa Rais William Ruto ambaye serikali yake inatekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu ambazo hatimaye zinauziwa raia.
Bw Mawaura pia alihudumu kama mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi katika Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambayo Dkt Ruto alitumia kushinda uchaguzi wa urais Agosti 9, 2022.
Umiliki wa hisa wa familia ya Mwaura katika HF ni kupitia kampuni za Toddy Civil Engineering, Effort Merchants na Janton Investments.
Mapema mwaka huu, Bw Ichung’wah kupitia mahojiano na shirika la habari la Al Jazeera alifuchua kuwa anamiliki mali ya thamani ya Sh1 bilioni.
Aliingia Bungeni mnamo 2013 na anahudumu muhula wake wa tatu kama mwakilishi wa eneo bunge la Kikuyu.