Ida akubali uteuzi wa Ruto, asema ni heshima kubwa
IDA Betty Odinga, mkewe aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga Jumapili alitangaza kuwa amekubali uteuzi wake kama Balozi wa Kenya katika Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Mazingira (UNEP) akisema hatayumbishwa na vitisho anavyoelekezewa.
Rais Ruto mnamo Ijumaa alimteua Mama Ida kuwa balozi wa UNEP, wadhifa atakaochukua iwapo ataidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
Mbunge wa Budalang’i Ababu Namwamba ambaye alikuwa akishikilia nafasi hiyo alihamishwa kuhudumu kama Balozi wa Kenya nchini Uganda.
“Ninawashukuru wale ambao wamenipongeza kwa sababu kwangu hii ni tunu. Hakuna mtu atanitishia wala kunitia uoga kwa sababu Mungu ndiye mchungaji wangu,” akasema akinukuu Kitabu cha Zaburi kwenye bibilia.
Mama Ida alisema kufiwa na mumewe na uteuzi kama balozi wa UNEP ni kati ya changamoto ambazo zinamwandama ila atasalia imara katika imani yake ya Kikristo.
“Ninaongea kwa ujasiri kwa sababu Mungu yuko nami na ananiandaliwa meza mbele ya watesi wangu. Kila mara nikiwasha runinga ama kufungua gazeti, ni Ida Odinga, sitaogopa kwa sababu Mungu hajanitelekeza,” akaongeza.
Kukubali uteuzi huo kulitokea wakati ambapo baadhi ya viongozi wa ODM na upinzani wamemtaka aukatae.
Wachanganuzi wanasema.
Mnamo Jumamosi, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi ambaye ni naibu kiongozi wa ODM alisema wadhifa huo ni mdogo kwa mtu wa hadhi ya Mama Ida.
“Tunamwomba mama wetu mpendwa Ida akatae wadhifa huo. Ida ni mtu maarufu anayehitaji wadhifa wa juu zaidi,” akasema Bw Osotsi.
Naye Naibu Kiongozi wa DCP, Cleophas Malala alisema uteuzi huo hauna maana akisema akina mama nchini wanapambana na changamoto mbalimbali ambazo zinastahili kushughulikiwa.
“Rais Ruto aliahidi kuwainua akina mama na kubuni nafasi za ajira. Badala ya kutekeleza ahadi hiyo, amemteua Mama Ida,” akasema Bw Malala katika mkutano wa kisiasa katika eneo la Kirinyaga.
Hata hivyo, Mama Ida amepata uungwaji kutoka kwa wafuasi wa ODM akiwemo kiongozi wa vijana Brian Omondi.
Bw Omondi pamoja na Rosemary Odinga waliapa kuwa kitengo cha vijana katika ODM kitamuunga mkono Mama Ida.
“Tumefurahishwa na uteuzi huu na kama vijana tunataka kuwaona vijana na wanawake wakiinuliwa kimaisha. Mama Ida amesema hatatishwa na sisi tutamuunga mkono,” akasema Bw Omondi, mwanawe aliyekuwa mbunge wa Gem marehemu Jakoyo Midiwo ambaye analenga ubunge wa Lang’ata mnamo 2027.
Kwenye hafla tofauti, viongozi wa ODM wanaompinga Dkt Oburu Oginga wameendelea kushinikiza chama hicho kiandae Kongamano la Kitaifa la Wajumbe (NDC) ili kuwateua maafisa wapya.
Viongozi hao ambao walihudhuria ibada ya kanisa katika mtaa wa Kawangware pia walisema jaribio lolote la kumfukuza Katibu Mkuu Edwin Sifuna halitafaulu.
“Ningependa kuwaambia kuwa iwapo mtu atathubutu kumfukuza au kumwondoa Sifuna kama katibu mkuu, huo utakuwa mwisho wa ODM,” akasema Gavana wa Siaya, James Orengo.
Gavana huyo pia alisisitiza kuwa familia ya Raila Odinga pamoja na watoto wake lazima waheshimiwe.
Bw Orengo alisema matamshi ya kweli ya marehemu Raila yako katika mambo aliyoyasema akiwa hai na maandishi yaliyomo katika ajenda 10 ambazo ODM ilitia saini na UDA.
Alisema Bw Sifuna alikuwa kati ya waliotia saini hoja hizo 10 kwa hivyo anafahamu anachokisema iwapo anaibua malalamishi.
Gavana huyo alisema muafaka kati ya ODM na UDA ulikuwa wa kushusha gharama ya maisha na si kuunda muungano wa kisiasa.
“Kwa hivyo, msidanganywe kwa sababu Raila hakusema chochote kuhusu kuungana kisiasa na yeyote. Alisema haki za Wakenya ndizo zipewe umuhimu kisha baadaye ndipo angeamua kuhusu mwelekeo wa kisiasa,” akasema Bw Orengo.
Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino alimuunga mkono Bw Orengo akisema hakukuwa na muafaka kati ya Raila na Rais Ruto kuhusu 2027.
“Ni vyama hivyo ndivyo vilimjia na kama wandani wake tutasimama na kile alichosema kinachofahamika wazi,” akasema Bw Owino.
Bw Osotsi naye alisema ODM ni chama cha Wakenya na hawatakubali kimezwe kutimiza maslahi ya viongozi wachache.