Habari za Kitaifa

IEBC: Imani duni ya Wakenya imefanya uchaguzi kuwa ghali zaidi

Na DAVID MWERE October 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Erastus Ethekon, amefichua kuwa ukosefu wa imani miongoni mwa Wakenya ndio sababu kuu ya uchaguzi kuwa miongoni mwa ghali zaidi Afrika na duniani.

Bw Ethekon alitoa kauli hiyo kwa Taifa Leo wakati ambapo tume hiyo imetengewa Sh10.46 bilioni kuandaa chaguzi ndogo za Novemba 27, 2025 katika maeneo ya uchaguzi 24. Aidha, IEBC inashinikiza kupewa angalau Sh61 bilioni ili kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.

Sehemu kubwa ya fedha hizo zitatumika kununua vifaa vya KiEMS takribani 46,000, marupurupu ya maafisa wa uchaguzi na usalama, uchapishaji wa karatasi za kura zenye usalama wa hali ya juu, na masuala ya uchukuzi miongoni mwa mengine.

“Hili suala la ukosefu wa imani linatufanya kuwa na wasiwasi mkubwa. Siku ambayo tutaitisha kikao kama Wakenya na tuwe na imani, tutafurahia kwa sababu tutapunguza gharama—kwa mfano, tunaweza kuchapisha karatasi za kura humu nchini badala ya kuagiza kutoka nje ilhali tuna uwezo huo,” alisema Bw Ethekon.

Zaidi ya gharama, Bw Ethekon alisema kuwa uchaguzi nchini Kenya unapingwa zaidi kisheria kuliko nchi nyingine za Afrika Mashariki na maeneo mengine duniani.

“Kwa nini hatuamini mifumo yetu? Tumeweka sheria na kanuni nyingi ili kudhibiti wasiwasi wetu kuhusu uwazi na uwajibikaji. Lakini je, hizi sheria zote zinatuhudumia au ni mzigo?” alihoji Mwenyekiti huyo wa IEBC.

Katika uchaguzi wa 2022, IEBC ilitumia Sh44.18 bilioni, sawa na takribani Sh2,200 au dola 20 kwa kila mpiga kura aliyejiandikisha. Hii ni zaidi ya viwango vya kimataifa vya dola 5 (takriban Sh646) kwa kila mpiga kura.

Kenya ilikuwa ya pili duniani kwa uchaguzi wa gharama kubwa, nyuma ya Papua New Guinea pekee, ambako uchaguzi uliwagharimu raia Sh6,300 au dola 48.84. Mwaka 2017, gharama ilikuwa karibu Sh2,000 kwa kila mpiga kura.

Wakati huo huo, Ghana ina uchaguzi wa bei nafuu zaidi barani Afrika kwa dola 0.07 kwa kila mpiga kura. Rwanda ilitumia dola 1.05 kwa kila mpiga kura mwaka 2017, Uganda dola 4, Tanzania dola 5.16, na Nigeria dola 8.61.

Kwa mujibu wa Bw Ethekon, gharama ya juu ya uchaguzi nchini Kenya inatokana na matakwa yanayoweza kuepukika iwapo Wakenya watajenga imani kwa taasisi zao.

Alieleza kuwa kila karatasi ya kura ina alama 11 za kiusalama, jambo linaloifanya kuwa salama zaidi kuliko hata noti za pesa za Kenya. Alisema awali noti za Kenya zilichapishwa nchini kabla ya kazi hiyo kupewa kampuni ya kigeni.

“Tuna uwezo wa kuchapisha karatasi za kura hapa nchini kwa bei nafuu na bado zikatekeleza madhumuni yake. Lakini kwa sababu hatujiamini, tunawaleta wageni,” alisema.

Anne Nderitu, Kamishna wa IEBC anayesimamia Elimu ya Mpiga Kura, alieleza kuwa ukosefu wa imani huathiri hata maafisa wa uchaguzi, kiasi kwamba wanashukiwa wakitumia magari ya serikali.

“Ni suala tunalopaswa kulishughulikia. Wenzetu wanatumia rasilmali za serikali kama magari ya umma wakati wa uchaguzi na hivyo kupunguza gharama,” alisema Bi Nderitu.

Sheria ya Uchaguzi inasema kuwa kituo kimoja cha kupigia kura kinapaswa kuwa na wapiga kura wasiozidi 700 ili kuepuka msongamano na kuharakisha mchakato wa upigaji kura.

Katika uchaguzi mkuu wa 2022, vituo vya kupigia kura 46,000 vilikuwa vimesajiliwa rasmi. Kufikia 2027, idadi hiyo inaweza kufika au kuzidi 50,000.

Hii ina maana kuwa kila kituo kitahitaji maafisa wake wa uchaguzi—maafisa ambao lazima walipwe.

Koki Muli, mtaalamu wa masuala ya uchaguzi, anasema kuwa IEBC inaweza kupunguza idadi ya vituo vya kupigia kura hadi nusu kwa kuruhusu wapiga kura 2,000 kwa kituo bila kuhitaji mabadiliko ya kisheria kutoka Bunge.

Usafiri pia umetajwa kama chanzo kikuu cha gharama ya juu ya uchaguzi. IEBC kwa sasa hulazimika kuajiri magari kutoka kwa kampuni binafsi kwa sababu hakuna imani ya kutumia magari ya serikali kwa ajili ya kusafirisha vifaa vya uchaguzi au maafisa wa tume hiyo.

“Kutokuwepo kwa imani katika kutumia magari ya serikali wakati wa uchaguzi kunamaanisha kuwa IEBC italazimika kukodisha magari ya kibinafsi kwa bei ya juu,” aliongeza Bi Nderitu.

Mule Musau, Mratibu wa Kitaifa wa kundi la waangalizi wa uchaguzi nchini anasema kuwa IEBC inatumia vituo vya kupigia kura kama vyanzo vya gharama.

“Tuna wasiwasi kuwa uchaguzi wetu ni ghali mno. Tunahitaji kupunguza vifaa vya usafiri na idadi ya wafanyakazi,” alisema Bw Musau.

“Iwapo tungetumia magari ya serikali kusafirisha vifaa na kuwa na maafisa wawili pekee kwa chaguzi za wadi, gharama hiyo ingepungua sana,” alisema na kuongeza kuwa hata makadirio ya kesi zinazotarajiwa nayo huwa ya juu sana.