• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
IEBC: Mswada wa kuajiri marefarii wa uchaguzi watua bungeni

IEBC: Mswada wa kuajiri marefarii wa uchaguzi watua bungeni

NA CHARLES WASONGA

MSWADA utakaofanikisha kuteuliwa kwa mwenyekiti na makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), umewasilishwa bungeni.

Huu ni utaratibu unaolenga kujaza nafasi ya mwenyekiti aliyestaafu Wafula Chebukati na makamishna sita wa tume hiyo.

Kwanza, mswada huo unaodhaminiwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah unapendekeza kubuni jopo jipya la kuendesha mchakato huo kulingana na mapendekezo ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco).

Jopo hilo jipya lenye wanachama tisa, litachukua nafasi ya jopo lililoteuliwa Machi 2, 2023, linaloongozwa na Nelson Makanda.

“Kando na hayo, mswada huu unalenga kusuluhisha mapungufu yaliyoko katika sheria ya sasa kwa kuweka kipindi mahususi cha kukamilishwa kwa shughuli hiyo,” akasema Bw Ichung’wah.

Kiongozi huyo alisema wameweka muda maalum wa kazi hiyo na jopo jipya litakalobuniwa litahitajika kukamilisha shughuli hiyo ya uteuzi wa mwenyekiti na makamishna wa IEBC ndani ya siku 90.

“Kuanzia siku ambayo wanachama wa jopo hili watateuliwa, sharti wakamilishe kazi ndani ya muda huo na kuwasilisha majina ya walioteuliwa kwa rais,” akaeleza.

Ripoti ya Nadco ilipendekeza kuwa jopo hilo jipya liwe na wanachama tisa “ili kuhakikisha kuwa maoni mengi na watu kutoka makundi zaidi ya washikadau wanahusishwa.”

Kulingana na Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya IEBC ya 2024, Bunge la Kitaifa limepewa mamlaka ya kuongeza kipindi cha kuhudumu kwa jopo hilo endapo “patatokea haja yenye mashiko.”

Kando na Dkt Makanda, wanachama wengine wa jopo la sasa ni Bi Charity Kisotu ambaye ni naibu mwenyekiti (na anayewakilisha Tume ya Utumishi wa Umma-PSC).

Wengine ni Fatuma Saman (ambaye pamoja na Dkt Makanda wanawakilisha Baraza la Madhehebu Nchini), na Evans Misati (anayewakilisha Kamati Shirikishi ya Vyama vya Kisiasa).

Aidha, Bethuel Sugut na Novince Atieno wanawakilisha Tume ya Huduma za Bunge (PSC) huku Benson Ngugi akiwakilisha Chama cha Wanasheria Nchini (LSK).

Wanachama wawili ambao wameongezwa katika jopo hili kulingana na mswada huu mpya ni mmoja atakayewakilisha Taasisi ya Wahasibu Nchini (ICPAK) na mwingine zaidi atakayewakilisha Kamati Shirikishi ya Vyama vya Kisiasa (Political Parties Liasion Committee).

  • Tags

You can share this post!

Jamii ya Wakore hatarini kumezwa kabisa na makabila mengine

LSK yaonya kuhusu hatari ya kusafiria gari lisilo na bima

T L