IEBC: Naam, tunachukua mboni ya jicho lako; iko sahihi kuliko alama za vidole
HUKU Tume Huru ya Uchaguzi Nchini (IEBC) ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027, Wakenya na wanasiasa wameibua masuali kuhusu teknolojia ambayo itatumika kwenye kura hiyo, mojawapo ikiwa ile ambayo inanasa mboni ya jicho.
Mnamo Septemba 29, 2025, IEBC ilianza kuwasajili wapigakura ambapo imekuwa ikiwalenga zaidi ya wapigakura wapya milioni 6.3 (wengi wao wakiwa wapigakura vijana) wakilenga kuongeza idadi ya wale ambao wamesajiliwa hadi milioni 28.7 kufikia mnamo 2027.
Usajili huo wa wapigakura kwa sasa unaendelea kwenye maeneobunge 278 pamoja na vituo 57 vya Huduma.
IEBC pia inatumia vifaa vya kielektroniki pamoja na vingine kuhakikisha kuna usawa katika usajili wa wapigakura.
Hata hivyo, teknolojia ambayo inanasa mboni ya jicho imegeuka kuwa gumzo kuu huku baadhi wakipinga kutumika kwake na wengine wakiunga.
Kwa mujibu wa Mtaalamu wa Teknolojia katika IEBC, Bw Gedfrey Ngunyi, kunasa mboni ya jicho kunaongezea tu matumizi ya teknolojia ya kielektroniki ambapo pia alama za vidole huchukuliwa.
“Mboni ya jicho ya kila mtu ina upekee wake wala si kama alama za vidole ambazo hutofautiana kwa sababu ya kutegemea kazi ambayo kila mtu hufanya,” akasema Bw Ngunyi.
Alifichua kuwa teknolojia hiyo itakuwa ikitumika kutambua mpigakura pale ambapo vidole vitakosa kutambuliwa na mashine ya kielektroniki.
“Inaruhisiwa kwenye sheria za uchaguzi na itasaidia katika kuhakikisha kuwa kuna uchaguzi ambao una uwazi mkubwa,” akaongeza.
Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuwaelimisha wapigakura Joyce Ekuam naye alifichua kuwa wapigakura wanaojisajili hunaswa mboni ya jicho kwa hiari yao wala huwa hawalazimishwi.
“Ndiyo mfumo huu upo lakini si wa lazima. Iwapo unahisi si sawa, basi unaweza kutambuliwa kielektroniki tu ambayo ni njia ya kawaida. Tunalenga tu kuhakikisha kuwa mchakato wa kuwatambua wapigakura unaimarishwa zaidi,” akasema Bi Ekuam.
Mwenyekiti wa IEBC, Bw Erastus Ethekon kwenye mahojiano na Taifa Leo alisema kuwa data za wale ambao mboni za macho yao zimenaswa zitahifadhiwa salama.
“Kupata maelezo ya wapigakura kutadhibitiwa na yeyote ambaye atavuruga na kutumia data hiyo vibaya, atachukuliwa hatua kali za kisheria,” akasema Bw Ethekon.
Mwenyekiti huyo wa IEBC aliwahakikishia Wakenya na wanasiasa kuwa teknolojia ambayo itatumika katika uchaguzi huo haitavurugwa na itakuwa na uwazi mkubwa.
“Mitandao na vyombo ambavyo tutatumia vina viwango vya juu vya usalama. Nawahakikishia Wakenya kuwa tutawajibika kwa kutekeleza jukumu la tume bila hofu yoyote na uchaguzi utakuwa huru na wenye haki,” akasema Bw Ethekon.
Kufikisha wapigakura wapya milioni 6.3, IEBC imetekeleza mabadiliko ambapo si lazima Mkenya ajisajili katika kituo kile ambako atapigia kura.
Kwa mfano mtu akifanya kazi Nairobi, Mombasa au Nakuru lakini wanataka kupiga kura mashinani, watachagua tu na kupiga kura kutoka mahali popote walipo.