IEBC: Wanasiasa ndio walivuruga chaguzi ndogo
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetoa taarifa kuhusu matokeo ya chaguzi ndogo za Novemba 2025, ikieleza mafanikio na changamoto zilizojitokeza wakati wa shughuli hiyo.
Katika mkutano wa wadau uliofanyika Nairobi hapo Jumatatu, Tume ilitoa tathmini ya chaguzi hizo na kuangazia maandalizi yake kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027.
Mwenyekiti wa IEBC, Erastus Ethekon, alifichua kuwa baadhi ya wanasiasa walijaribu kuingilia mchakato wa uchaguzi kwa nia ya kubadilisha matakwa ya wananchi.
Alitaja kuwepo kwa changamoto za kutojitokeza kwa wapigakura, utoaji na ulaji rushwa, kuvurugwa kwa shughuli katika vituo vya kupigia kura pamoja na matumizi ya magenge ya wahuni kuwatisha wapigakura na maafisa wa IEBC.
Bw Ethekon alieleza wasiwasi wake kuhusu kupungua kwa idadi ya wapigakura, akisema hali hiyo inatishia misingi ya demokrasia nchini.
“Haikuanza na chaguzi hizi ndogo. Mnamo 2017, ushiriki wa wapiga kura ulikuwa asilimia 78.9, ukashuka hadi asilimia 64.4 mwaka wa 2022 na uchaguzi mdogo wa 2025 umeonyesha mwenendo huo unaendelea,” akasema.
Bw Ethekon alisema tatizo hilo haliko kwa IEBC pekee, kwani mara nyingi vyama vya kisiasa na wagombea huwatisha wapiga kura kisha kulaumu IEBC kwa idadi ndogo ya waliojitokeza.
Alisisitiza haja ya mjadala wa kitaifa kuhusu sababu zinazosababisha kutojitokeza kwa wapiga kura, hususan vijana.
Mwenyekiti huyo pia alifichua kwamba kulikuwa na majaribio ya wanasiasa kuingilia mchakato wa uchaguzi kwa kushawishi maafisa wa Tume kupendelea wawaniaji.
Alisisitiza kwamba Tume imejikita kuhudumia nchi kwa kutenda haki bila upendeleo, na haitavumilia uvurugaji wa aina yoyote.
Bw Ethekon alilaani vitendo vya utoaji na ulaji hongo, unyanyasaji na vitisho dhidi ya wasimamizi wakuu na wasimamizi wa kura, akishangazwa na wanasiasa wanaodai kuwa maarufu kugeukia matumizi ya mbinu hizo.
Aliwataka wanasiasa kukubali matokeo ya uchaguzi badala ya kutafuta ushindi kwa njia zisizo halali.
Aidha, Bw Ethekon aliripoti matukio ya kushambuliwa kwa maafisa wa IEBC na uharibifu wa vifaa vya uchaguzi katika baadhi ya vituo, akisema vituo sita viliathiriwa.
Alibainisha kuwa wahuni walitumwa kusababisha vurugu na hali ya taharuki ili kukwamisha upigaji kura.
Alikosoa pia tabia ya baadhi ya wanasiasa waliowasili katika vituo vya kupigia na kuhesabu kura wakiwa na wafuasi, hali iliyosababisha usumbufu.
Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan, alieleza kuwa chaguzi hizo ndogo zilikuwa za kipekee na zilitoa mwanga kuhusu utayari wa IEBC katika masuala ya kiutendaji, kiteknolojia na ushirikishwaji wa wadau.
Licha ya kufanikiwa kwa chaguzi hizo, alikiri kuwepo kwa changamoto kama kutojitokeza kwa wapiga kura, utekelezaji wa vifaa, upotoshaji wa taarifa na matukio machache ya ukosefu wa kiusalama.
Alisema mambo hayo yanaonyesha kwamba usimamizi wa uchaguzi ni safari endelevu ya kujifunza.
Tume ilifichua pia kuwa ilipokea malalamiko tisa kuhusu wagombea waliopitishwa kuwania nafasi mbalimbali; sita yalitatuliwa na Tume huku matatu yakiwasilishwa mahakamani.
Kwa ujumla, IEBC imesisitiza kujitolea kwake kwa uwazi, weledi na kulinda uadilifu wa chaguzi nchini Kenya, huku ikitaka wanasiasa na wananchi kushirikiana kuimarisha demokrasia na kuhakikisha chaguzi huru na haki.