Habari za Kitaifa

IEBC yafungulia uwanja Raila, Ruto, Gachagua kumenyana

Na  JUSTUS OCHIENG August 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetangaza kuwa chaguzi ndogo 24 zinazosubiriwa kwa muda mrefu zitafanyika Novemba, 27 2025, na hivyo kumaliza miezi ya ukosefu wa uwakilishi katika maeneo husika.

Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, IEBC ilisema uchaguzi huo mdogo utafanyika kwa awamu mbili, ambazo zitachapishwa katika gazeti rasmi la serikali mwezi huu. Hali hii imefungua uwanja wa mapambano ya kisiasa yanayotarajiwa kuhusisha Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga, na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ambaye sasa anaongoza muungano mpya wa upinzani.

Awamu ya kwanza ya tangazo hilo, iliyochapishwa Ijumaa Agosti 8, inahusisha Wadi 16 katika kaunti 12, zikiwemo Angata Nanyokie (Samburu), Chemundu/Kapng’etuny (Nandi), Chewani (Tana River), Fafi (Garissa), Kariobangi North (Nairobi), Kisa East (Kakamega), Metkei (Elgeyo Marakwet), Mumbuni North (Machakos), Narok Town (Narok), Purko (Kajiado), Tembelio (Uasin Gishu), Nyansiongo, Nyamaiya, na Ekerenyo (Nyamira), Lake Zone na Nanaam (Turkana).

Awamu ya pili itachapishwa Jumatatu Agosti 11, na itahusisha kiti kimoja cha Seneti (Baringo), viti sita vya Bunge la Kitaifa: Banissa, Kasipul, Magarini, Malava, Mbeere North na Ugunja, na kiti kimoja cha MCA cha wadi ya Kabuchai/Chwele (Bungoma).

Baadhi ya maeneo haya hayajakuwa na viongozi kwa zaidi ya miaka miwili kutokana na ushindi wao kubatilishwa mahakamani au vifo vya waliokuwa wakiyawakilisha.

Mwenyekiti mpya wa IEBC Bw Erastus Ethekon Jumatano alisema kamati ya uchaguzi ya tume hiyo inakamilisha ratiba kamili ya chaguzi zote ndogo za mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 101(4)(b), uchaguzi mdogo unapaswa kufanyika ndani ya siku 90 baada ya viti kutangazwa kuwa wazi, isipokuwa iwapo nafasi hiyo inatokea ndani ya miezi sita kuelekea uchaguzi mkuu.

Tangazo hili linawasha joto la kisiasa, huku vyama vikuu vikijiandaa kupimana nguvu. Chama cha UDA cha Rais Ruto kinalenga kuonyesha nguvu yake mashinani, huku ODM cha Bw Odinga kikijaribu kulinda ngome zake za jadi.

Ingawa wawili hao kwa sasa wanaonekana kushirikiana kunsa uwezekano wa kufikia makubaliano ya kugawana maeneo kadhaa.

Kwa upande mwingine, Rigathi Gachagua ambaye anajitokeza kama kiongozi wa upinzani mpya unaopinga Ruto na Raila kwa pamoja, anatarajiwa kutumia uchaguzi huu mdogo kupima nguvu za kisiasa za kundi lake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.