IEBC yajitetea kuhusu jina la Wamuthende katika uchaguzi mdogo Mbeere Kaskazini
TUME ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeomba Mahakama Kuu itupilie mbali kesi inayopinga ushindi wa Mbunge wa Mbeere North, Leo Wa Muthende, ikisema kuwa uchaguzi mdogo wa Novemba 27 ulikuwa halali na tofauti zozote za majina hazingeepukika wala hazikuathiri matokeo.
Stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani na IEBC pamoja na msimamizi wa uchaguzi wa eneo bunge la Mbeere North, zinaweka msingi wa kutetea uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba 27, 2025.
Wanakanusha madai ya udanganyifu, upotoshaji au kasoro zozote yaliyoibuliwa na wapiga kura wawili waliowasilisha kesi mahakamani siku chache baada ya matokeo kuchapishwa katika Gazeti Rasmi la Serikali.
Kesi hiyo inapinga ushindi wa Leo Wa Muthende Njeru, ambaye awali alijulikana kama Leonard Muriuki Njeru.
Walalamishi, Julieta Karigi na Patrick Gitonga, wanadai kuwa mabadiliko ya jina lake na kuendelea kuonekana kwa jina lake la zamani katika sajili ya wapiga kura na baadhi ya nyenzo za uchaguzi kulihatarisha uchaguzi huo.
Wanataka ushindi wa mbunge huyo ubatilishwe na uchunguzi huru wa nyezo za uchaguzi ufanyike. Wanasema mshindi alishiriki akitumia majina tofauti kwenye kumbukumbu za wapiga kura na karatasi za uchaguzi.
Hata hivyo, katika majibu ya kesi, IEBC na msimamizi wa uchaguzi wanasema mgombeaji huyo alibadilisha jina lake kisheria kabla ya uteuzi na kwamba uchaguzi huo mdogo ulizingatia Katiba na sheria za uchaguzi, na uliakisi chaguo la wapiga kura.
Wanasema kuendelea kuonekana kwa jina lake la zamani kulitokana na kusitishwa kisheria kwa mabadiliko yoyote katika sajili ya wapiga kura.
“Majina mawili hayakuathiri utambulisho wake au sifa zake, wala hayakumdhuru mpinzani yeyote au wapiga kura,” anasema wakili wa washtakiwa, Bw Charles Mwongela.
Stakabadhi za kesi zinaeleza kuwa sajili ya wapiga kura ilisitishwa mara tu tarehe ya uchaguzi mdogo ilipotangazwa, hivyo jina la Bw Wa Muthende halingeweza kubadilishwa.
“Hakuna mabadiliko yoyote, yakiwemo ya majina au maelezo ya wapiga kura, yaliyoruhusiwa kufanywa,” wakili anasema, akieleza kuwa sajili ilipaswa kubaki kama ilivyokuwa Juni 21, 2022.
“Aidha, kuendelea kuwepo kwa jina la awali la mshtakiwa wa kwanza katika Sajili ya Wapiga Kura na nyenzo za uchaguzi kulikuwa halali, hakungeepukika na hakukuwa na madhara kwa walalamishi,” anaongeza.
Walisema pia kuwa Bw Wa Muthende aliwasilisha stakabadhi zote zilizohitajika wakati wa uteuzi, ikiwemo hati ya kubadilisha jina na notisi ya Gazeti Rasmi kuthibitisha mabadiliko hayo.
Pia, kulingana na wakili Mwongela, alitambuliwa kwa kutumia kifaa cha KIEMS kama mpiga kura aliyesajiliwa Mbeere North na akaidhinishwa baada ya kutimiza masharti yote ya kisheria.
“Wagombeaji wote walipitia vigezo sawa,” anasema wakili na kuongeza kwamba kutambuliwa kisheria kulithibitisha kikamilifu maelezo ya mpiga kura kabla ya kuidhinishwa.
IEBC inaeleza kuwa karatasi za kura zilikuwa na jina la mgombeaji, alama ya chama na picha yake. Ikirejelea uamuzi wa awali wa mahakama, tume inasema suala la jina lina uzito tu endapo linaweza kuwachanganya wapiga kura hadi wakampigia kura mtu asiye sahihi.
IEBC ilitangaza rasmi uchaguzi mdogo Agosti na kuweka ratiba za uteuzi, kampeni na upigaji kura. Sajili ya wapiga kura iliyotumika ilikuwa ile iliyoidhinishwa Juni 2022 kabla ya uchaguzi mkuu uliopita.
Stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa siku ambayo wagombea wa Mbeere North walikuwa wakiidhinishwa Oktoba 2025, msimamizi wa uchaguzi, John Mwii Kinyua, alikuwa amelazwa hospitalini.
Alikabidhi majukumu hayo kwa naibu msimamizi wa uchaguzi, Curtis Mawira Njeru, hatua ambayo IEBC inasema ilikuwa halali chini ya kanuni.
Kesi imepangwa kusikilizwa Januari 15, 2026.