IEBC yataka Sh3.5 bilioni kujenga makao makuu
TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) sasa inalenga kujenga makao makuu mapya kwa kima cha Sh3.5 bilioni.
Ujenzi huo ukifaulu utashuhudia wakihama makao makuu yao ya sasa kwenye Jumba la Anniversary Towers katikati mwa jiji la Nairobi.
Kwa mujibu wa IEBC, mpango huo unahusisha ujenzi wa Jumba la Uchaguzi ambalo linatarajiwa kuanza Julai 2026 iwapo kutakuwa na fedha za kutosha.
Afisa Mkuu Mtendaji wa IEBC Marjan Hussein Marjan alisema tume hiyo inatarajia itapata fedha kufadhili ujenzi huo mwaka wa kifedha wa 2026/27.
Akiwa mbele ya Kamati ya Haki na Sheria, Bw Marjan alisema kuwa wanatarajia Sh201 milioni kwenye mwaka wa kifedha unaokamilika 2027 kisha Sh602 milioni mwaka utakaofuata wa 2027/28.
“Kuwa na makao makuu kutapunguza gharama inayoelekezwa katika kulipa kodi ya afisi, maeneo ya shughuli mbalimbali kama mikutano na washikadau pamoja na wawaniaji kisha pia mafunzo kwa wafanyakazi na washikadau,
“Kwa kifupi kuwa na makao makuu ya IEBC kutawaepushia Wakenya mzigo mkubwa wa kufadhili gharama na shughuli za tume,” akasema Bw Marjan mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Bomet Hillary Sigei.
Mnamo Machi 16, 2021, IEBC ilitangaza tenda ya kununua ardhi ambako makao makuu yake yangejengwa. Ilisema kuwa ardhi hiyo lazima ipatikane kilomita 20 kutoka katikati mwa jiji na lazima iwe rahisi kufikia kupitia barabara.
“Ardhi hiyo lazima iwe ekari tano na iwepo eneo tambarare,” ikasema maelezo kwenye tenda hiyo.
IEBC imekuwa ikitumia zaidi ya Sh100 milioni kila mwaka kulipa kodi kwa afisi zake Anniversary Towers ambayo inamilikiwa na Kenya Re.
Jengo hilo limetumiwa na tume kwa zaidi ya miaka 20 na kiwango hicho cha kodi hakijumuishi gharama nyingine ya kukodisha maeneo ya kufanyia mikutano na kuandaa mafunzo.
Juhudi za kuhamisha IEBC zilianza 2013 wakati ambapo Isaac Hassan alikuwa mwenyekiti. Wakati huo tume hiyo ilitaka itengewe Sh800 milioni kununua jumba ambalo lingekuwa afisi zake huku ikisikitikia kodi ya Sh48 milioni kila mwaka.
Bw Hassan aliambia Bunge kuwa Anniversary Towers ilikuwa na msongamano na kuwa hatari kwa wafanyakazi wake. Mrithi wake Wafula Chebukati alifufua juhudi hizo mnamo 2018 akisema maandamano ya mara kwa mara yalikuwa yakivuruga shughuli za tume hiyo.
Mnamo 2017 aliyekuwa Mbunge wa Starehe Charles Njagua aliitaka IEBC ihamie Bomas of Kenya akisema maandamano dhidi ya tume hiyo wakati huo yalikuwa yakivuruga shughuli zake jijini.