Habari za Kitaifa

IG Masengeli azidi kukaidi korti kueleza waliko vijana waliotoweka wakati wa maandamano ya Gen Z

Na RICHARD MUNGUTI September 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAHAKAMA Kuu imemwamuru Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi, IG, Gilbert Masengeli afike kortini mwenyewe kujitetea kabla ya kuadhibiwa kwa kudharau maagizo ya korti.

Jaji Lawrence Mugambi alimwagiza Bw Masengeli afike kortini kuomba msamaha kwa kukaidi maagizo matatu ya mahakama kabla kesi ya kueleza waliko ndugu wawili na mwanaharakati Boby Njagi waliko.

Ndugu hao Jamal Longton Hashim na Aslam Longton, pamoja na Njagi walitoweka Agosti 19, 2024 kutoka makazi yao mjini Kitengela.

Kufikia sasa, Jaji Mugambi alisema familia za watatu hao hazijui waliko na wanaomba haki itendeke.

“Sheria inamtaka IG na kikosi chote cha polisi kihakikishe maisha ya kila Mkenya yamelindwa,” alisema Jaji Mugambi.

Jaji huyo alisema Masengeli amekaidi mara tatu kufika kortini kueleza waliko ndugu hao wawili na Njagi.

“Masengeli amekaidi maagizo ya hii mahakama mara moja Agosti na mara mbili Septemba 2024. Leo (Jummane, Septemba 4, 2024) hakuona ni jambo la maana kushiriki katika kesi hii kwa njia ya mtandao. Alasiri hakuona haja ya kufika kortini kama alivyoagizwa,” Jaji Mugambi alisema.

Jaji huyo alisema Masengeli ameidharau korti na kuikaidi.

“Nchi hii inatawaliwa na sheria wala sio wanaume wanaojihisi wako na mamlaka. Masengeli amekaidi sheria na hakuona haja afike kortini angalau kuweka wazi waliko ndugu hao waliotoweka bila ya kuonekana,” alisema Jaji Mugambi.

Jaji huyo alimpata na hatia Masengeli ya kukaidi maagizo ya mahakama.

Awali, Rais wa Chama Cha Mawakili Nchini (LSK) Faith Odhiambo aliomba mahakama imchukulie hatua kali Masengeli kwa kutoheshimu mahakama na kudharau mahakama.
Odhiambo alieleza Jaji Mugambi bayana kuwa Masengeli hana heshima yoyote kwa mahakama kwa vile amekaidi maagizo matatu yaliyotolewa Agosti na Septemba mwaka huu, 2024, akitakiwa kufika kortini kuelezea waliko ndugu hao wawili na mwanaharakati anayedaiwa kutekwa nyara na maafisa wa polisi waliokuwa wamevalia barakoa na nguo za raia wakati wa maandamano ya Gen Z
Odhiambo alieleza mahakama badala ya Masengeli kufika kortini kuelezea waliko watau hao waliotoweka yapata zaidi ya mwezi mmoja sasa, amemtuma wakili badala ya naibu wake kuelezea kilichojiri kuhusu watatu hao.

LSK iliwasilisha kesi mahakamani ikiomba Masengeli afike kortini kueleza waliko watatu hao.

Jaji Mugambi aliambiwa Afisa Mkuu katika Kituo cha Polisi cha Kitengela, aliambia Taifa Dijitali kwamba polisi walikuwa wamezuia Njagi.