Habari za Kitaifa

Ijumaa ni holidei, Rais Ruto atangaza

May 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

SERIKALI imetangaza kwamba Ijumaa, Mei 10, 2024, itakuwa siku ya mapumziko kuwakumbuka Wakenya waliopoteza maisha yao kutokana na janga la mafuriko lililosababishwa na mvua kubwa inayoshuhudiwa nchini.

Rais William Ruto ametangaza Jumatano kuwa siku hiyo pia itatumika kuendesha mpango wa kitaifa wa upanzi wa miti kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka kwa Wizara ya Usalama wa Ndani, jumla ya watu 238 wameaga dunia kutokana na madhara ya mvua hii, ilhali 75 hawajulikani waliko.

“Aidha, jumla ya familia 47,000 au watu 235,000 wameathirika katika janga hili huku watu 174 wakiwa ni wale waliojeruhiwa,” Waziri Kithure Kindiki akasema kwenye taarifa kuhusu hali ya janga hilo, Jumanne.

Mara ya kwanza serikali ya Rais Ruto kutangaza siku ya mapumziko kwa ajili ya Wakenya kushiriki upanzi wa miti ilikuwa ni Novemba 6, 2023.

Kwenye tangazo katika gazeti rasmi la serikali, waziri Kindiki alitangaza Novemba 13, 2023, kuwa siku ambayo Wakenya wangeshiriki shughuli ya kitaifa ya upanzi wa miti.

Shughuli hiyo iliyoongozwa na Rais Ruto mwenyewe katika Kaunti ya Makueni, ilishirikisha mawaziri na viongozi wengine wakuu serikalini kama sehemu ya juhudi za kutimiza azma ya serikali ya kuhakikisha kuwa miti 15 bilioni inapandwa nchini ndani ya miaka 10 hadi 2032.

Inakadiriwa kuwa hadi miche 150 milioni ya miti ilipandwa siku hiyo katika shughuli iliyoshirikishwa na Wizara ya Misitu na Wanyapori.