‘Itachukua serikali miaka 50 kupata pesa ambazo Adani itatumia kuboresha JKIA ndani ya miaka 30’
MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege nchini (KAA), itachukua miaka 50 kukusanya Sh200 bilioni ambazo Adani Airports Holdings Ltd inataka kuingiza katika upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, wabunge wameambiwa.
Katibu wa Uchukuzi, Bw Mohamed Daghar aliambia Kamati ya Bunge kuhusu Utekelezaji kwamba kampuni hiyo ya India inakusudia kuwekeza Sh200 bilioni katika kipindi cha makubaliano cha miaka 30.
Alisema KAA inazalisha Sh4 bilioni kama mapato halisi kila mwaka na itachukua miaka 50 ili kuboresha huduma katika JKIA.
“Adani inataka kuboresha JKIA kwa Sh200 bilioni kwa mkataba wa miaka 30. Hatuna uwezo wa kifedha wa kuwekeza pesa kama hizi. KAA hutengeneza mapato ya jumla ya Sh4 bilioni kila mwaka ilhali tunahitaji Sh200 bilioni ili kuendeleza miundombinu katika JKIA,” Bw Daghar aliambia wabunge.
“JKIA iliundwa kuhudumia abiria 7.6 milioni kila mwaka lakini kwa sasa tunahudumia 8.2 milioni. Itachukua KAA miaka 50 kuboresha miundombinu katika uwanja wa ndege.”
Bw Daghar aliambia kamati inayoongozwa na Mbunge wa Budalangi Raphael Wanjala kwamba serikali imechelewa kwa miaka 10 katika kuboresha majengo ya JKIA.
Alisema uwanja wa ndege ulikumbwa na kisa cha moto mnamo 2014, ujenzi uliopendekezwa wa Kituo cha Greenfield ulikatizwa, na JKIA kwa sasa ina msongamano.
“Adani Airports Holdings Limited itawekeza pesa bila serikali kulipa chochote,” alisema.
“Adani pia italipa ada za makubaliano kwa KAA katika kipindi cha miaka 30 hata kama watarudisha uwekezaji wao.”
Bw Daghar alikuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje aliyetaka kujua ikiwa mkataba wa Adani Airports Holding unapendelea shirika la ndege la Kenya Airways au utafungua JKIA kwa mashirika ya ndege kutoka India na Asia kushindana na shirika la ndege la kitaifa.
Bw Daghar alifika mbele ya kamati hiyo pamoja na Afisa Mkuu Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ndege la Kenya Alan Kilavuka na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KAA Henry Ogoye.
Bw Daghar alisema suala la Pendekezo la Ushirikiano wa Kibinafsi na Serikali la Adani Holdings Limited (PIP) kwa sasa liko katika Mahakama Kuu.
Mpango wa kukodisha JKIA kwa AAHL— kampuni tanzu ya Adani Group— ulizuka Julai mwaka huu.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA) iliidhinisha AAHL kwa siri kuchukua udhibiti wa JKIA, kabla ya agizo la mahakama kuzima mpango huo.