Habari za Kitaifa

Itumbi sasa atumia afisi rasmi za marais wastaafu

Na  JUSTUS OCHIENG’ August 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Majengo ya kifahari katika mtaa wa Nyari, Gigiri jijini Nairobi, yaliyonunuliwa kwa Sh250 milioni na serikali kuwa afisi rasmi ya marais wastaafu, sasa linatumika kama makao ya Mkuu wa Sekta ya Uchumi wa Ubunifu na Miradi Maalum katika Afisi ya Rais, Bw Dennis Itumbi.

Majengo hayo ya Nyari, yaliyonunuliwa mwaka wa 2013 kwa gharama iliyozua utata mkubwa, yalitumiwa kwa muda na aliyekuwa Rais Mwai Kibaki baada ya kustaafu, kabla ya kutelekezwa na mrithi wake, Rais wa nne Uhuru Kenyatta, aliyependelea kutumia afisi yake binafsi iliyoko Caledonia, karibu na Ikulu ya Nairobi.

Mwanzoni serikali ilipinga ombi  la Bw Kenyatta, lakini hatimaye ilikubali, na tangu wakati huo, afisi hiyo ya Nyari imekuwa wazi hadi ilipochukuliwa na Bw Itumbi mwaka jana.

Msemaji wa Ikulu, Bw Hussein Mohamed, alisema haikuwa sahihi kudai kuwa afisi hiyo ilikataliwa, akieleza kuwa marehemu Rais Kibaki aliitumia, na kwamba serikali iliruhusu Bw Kenyatta kutumia afisi ya chaguo lake.

“Afisi ya Nyari bado ipo wazi iwapo Rais mstaafu atabadilisha nia. Kwa sasa, imepewa matumizi mengine rasmi ya serikali badala ya kuachwa bila kazi,” alisema Bw Mohamed.

Kuhusu kwa nini afisi ya hadhi kama hiyo inatumiwa na afisa wa daraja la chini kama Bw Itumbi, Bw Mohamed alisema hilo ni suala la uwajibikaji wa matumizi ya mali ya umma.

“Ni busara kutumia majengo yaliyopo kwa kazi za serikali badala ya kuyaacha yakiwa tupu. Hakuna ubadhirifu wa mali ya umma katika hatua hii,” aliongeza.

Afisi hiyo iligharimu Sh250 milioni baada ya bajeti ya awali ya Sh700 milioni kwa afisi ya rais mstaafu kupunguzwa kufuatia ghadhabu ya umma. Kwa karibu muongo mmoja, Bw Kibaki aliitumia kabla ya kustaafu maisha ya umma.

Bw Itumbi amesema alihamishia shughuli zake katika majengo hayo kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuepuka kupoteza pesa za umma.

“Haifai kuacha jengo la serikali likiwa na wafanyakazi na vifaa bila kazi hadi 2032 kwa matumaini kuwa litatumiwa siku moja,” alisema Bw Itumbi. “Miundomsingi ya umma inapaswa kuhudumia umma.”

Alisema licha ya hadhi ya kihistoria ya jengo hilo, kazi ndiyo ya maana zaidi.

.