Jaji Mkuu Koome azingirwa na masaibu mawakili wakitisha kugomea mahakama
JAJI Mkuu Martha Koome anakumbwa na masaibu kufuatia kile alichotaja kama kuondolewa kwa walinzi wake na kupunguzwa kwa maafisa wa polisi wa mahakama, habari ambazo serikali na polisi walikanusha.
Mnamo Alhamisi jioni, Jaji Koome aliandikia Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen akilalamikia kuondolewa kwa walinzi wake na kupunguzwa kwa maafisa wa kitengo cha polisi wa mahakama.
“Kuondolewa kwa maafisa hawa wa usalama ni dharau kubwa kwa kanuni ya uhuru wa mamlaka. Hatua kama hiyo sio tu inadhoofisha imani katika taasisi za umma lakini pia inaweka historia hatari, kwamba ofisi kuu za kikatiba zinaweza kudhoofishwa kupitia shinikizo kutoka nje au kulipiza kisasi,” Jaji Koome alisema katika barua hiyo.
Hata hivyo, barua hiyo iliibua kitendawili huku Msemaji wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi Resila Onyango Alhamisi akisema maafisa hao waliitwa kuhudhuria mafunzo na kwamba nafasi zao zilikuwa zimechukuliwa na wengine.
Kilio cha Jaji Koome kiliashiria mzozo huku mahakama ikipigana vita vingi ambavyo sasa vinatishia kuyumbisha asasi hiyo muhimu.
Jana, Chama cha Wanasheria nchini Kenya (LSK) kiliunga Jaji Koome kulalamikia madai ya kuondolewa kwa maafisa wa usalama, lakini pia kikatishia kuongoza mgomo ikiwa Mahakama ya Juu anayoongoza Jaji Mkuu haitaondoa marufuku dhidi ya Wakili Ahmednasir Abdullahi.
Bw Murkomen alidai Jaji Mkuu alipiga nduru kuhusu suala ndogo huku akishikilia kuwa usalama wake uko sawa akiwa na maafisa wa polisi 29 kumlinda.
Bw Murkomen alisema maafisa watatu waliondolewa kwa muda ili kuhudhuria mafunzo wakisubiri kupandishwa vyeo katika Huduma ya Kitaifa ya Polisi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kitengo cha Polisi cha maafisa wa Utawala wa Serikali ya Kitaifa (NGAPU) huko Diani, Kaunti ya Kwale, Bw Murkomen alimkashifu Jaji Koome kwa kuandika barua ya kulalamika Alhamisi, ambayo nakala yake ilitumwa kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja.
Katika barua hiyo, Jaji Koome alilalamikia kuondolewa kwa walinzi wake bila mawasiliano yoyote, na kupunguzwa kwa maafisa katika Kitengo cha Polisi cha Mahakama.
Japo Jaji Koome hakutaja idadi kamili ya maafisa walioondolewa, Chama cha Mahakimu na Majaji wa Kenya Alhamisi kilidai kuwa maafisa 23 chini ya Kitengo cha Polisi cha Mahakama wameathirika.
“Maafisa wanapopandishwa vyeo, wanahitaji kupata mafunzo. Kwa bahati mbaya, Jaji Mkuu alijitokeza hadharani kuhusu suala hili. Hata hivyo, nilimhakikishia kwamba suala hilo lingetatuliwa. Hili lilikuwa suala dogo ambalo hakufaa kupiga nduru. Jaji Mkuu analindwa vya kutosha na takriban maafisa 29, na usalama wake, pamoja na ule wa majaji wengine, umehakikishwa,” Bw Murkomen alisema.
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Kenya, Faith Odhiambo alisema Ijumaa kuwa usalama kwa maafisa wa mahakama kama vile mihimili mingine miwili ya serikali hauwezi kujadiliwa.
LSK ilishutumu Mahakama ya Juu, ambako Jaji Koome ni rais, kwa kuendelea kuzima wakili Ahmednasir Abdullahi.Bi Odhiambo alitoa wito Mahakama ya Juu kuondoa marufuku kwa Bw Abdullahi la sivyo ikabiliwe na presha ikiwemo mgomo wa mawakili.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA