Habari za Kitaifa

Janga lakodolea macho mamilioni ya watoto serikali ikikosa kununua chanjo muhimu

May 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WAZIRI wa Afya, Susan Nakhumicha, amekiri kuwa kuna uhaba wa chanjo za watoto nchini na kusema wizara yake imetwika jukumu Kampuni ya Kimataifa ya Global (GAVI) kuwasilisha chanjo mbalimbali kuokoa hali.

Kauli ya Bi Nakhumicha inakuja wakati ambapo uongozi wa Baraza la Magavana Nchini (COG) umeibua wasiwasi kuhusu ukosefu wa chanjo muhimu nchini. COG imeitaka wizara iharakishe kuleta chanjo za watoto wanaozaliwa na wale ambao wapo chini ya umri wa miaka mitano.

Kaunti kadhaa tayari zimeathirika na ukosefu wa chanjo za watoto na kuwasababishia wazazi wasiwasi mwingi. Ukosefu wa chanjo umekwepo kati ya Machi na Mei.

Chanjo ambazo zimeisha katika kaunti ni zile za Polio (OPV&IPV), kifua kikuu (BCG), surua (MR) na pepopunda (Tetanus Diphtheria almaarufu Pentavalent).

Ukosefu wa chanjo hizo umeibua wasiwasi kuwa kutakuwa na ongezeko la polio na maradhi ya kifua kikuu.

Kwenye mahojiano na Taifa Leo, Bi Nakhumicha alikiri kuwa kuna uhaba wa chanjo nchini akisema kuwa hilo limesababishwa na kuvurugika kwa mpango wa uagizaji wa chanjo nchini.

Hata hivyo, alisema wizara yake inashughulikia suala hilo kidharura na chanjo zote zitakwepo humu nchini baada ya kipindi kifupi, japo hakufafanua hasa ni lini.

“Tunatoa chanjo katika kaunti ambazo zina visa visa vingi vya maradhi hadi zile ambazo zinashuhudia uhaba,” akasema Bi Nakhumicha.

Aliongeza kuwa mazungumzo yanaendelea na kampuni ya Gavi ili tatizo la uagizaji na usambazaji wa chanjo nchini lipate suluhu ya kudumu.

Mnamo Alhamisi, Mwenyekiti wa COG Anne Waiguru, aliandikia wizara hiyo akisema kuwa kuna ukosefu wa chanjo katika vituo mbalimbali vya afya na hospitali. Bi Waiguru alisema uhaba huo umesababisha wasiwasi hasa miongoni mwa wazazi wa watoto wanaozaliwa.

Aidha, imebainika kuwa Kenya imekosa kulipa deni la Sh2 bilioni kwa kampuni moja ya kimataifa iliyokuwa ikisambaza chanjo nchini na hilo ndilo limechangia uhaba wa sasa.

Takwimu zinaonyesha kuwa watoto ambao hawajazaliwa milioni 1.6 na wanawake wajawazito wapo hatarini kutokana na uhaba huo wa chanjo. Wasichana 750,000 ambao wapo chini ya umri wa miaka 10 pia wataathirika.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia, watoto ambao hupelekwa kliniki hawapewi chanjo katika Hospitali Kuu ya Kaunti ya Trans Nzoia, Kitale, na vituo vya afya vya Tom Mboya.

Watoto hao wamekuwa wakikosa chanjo ya polio na nyingine muhimu huku Gavana George Natembeya akithibitisha hali ni mbaya.

Katika Kaunti ya Turkana, Afisa Mkuu Mtendaji wa Hospitali ya Lodwar Dkt Joseph Epem, alisema kuwa katika muda wa mwezi mmoja uliopita, kumekuwa na uhaba wa chanjo ya kifua kikuu na polio.

Pia uhaba wa chanjo kwa watoto ambao wapo chini ya umri wa miaka saba iliriporitiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kapenguria, Kaunti ya Pokot Magharibi. Supritendanti wa hospitali hiyo, Dkt Simon Kapchanga, alisema chanjo nyingi za watoto hazipo.

Ripoti za Evans Jaola, Sammy Lutta na Oscar Kakai