• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Jaribio la Babu Owino kumng’atua Waziri Nakhumicha ni sawa na kukwea mlima kwa ‘slippers’

Jaribio la Babu Owino kumng’atua Waziri Nakhumicha ni sawa na kukwea mlima kwa ‘slippers’

NA CHARLES WASONGA

HUENDA nia ya Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino ya kumwondoa afisini Waziri wa Afya Susan Nakhumicha ikagonga mwamba kutokana na mseto wa sababu za kisiasa na kisheria.

Kwanza, kuna dalili zimeanza kuonyesha kuwa hoja hiyo itakosa uungwaji mkono serikalini na katika upinzani.

Sababu nyingine ni masharti magumu ya kisheria, yaliyowekwa na Spika wa zamani wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi 2015 kwa wabunge kutimiza kabla ya kuwasilisha hoja ya kumtimua waziri wa serikali.

Kwenye taarifa aliyotoa bungeni mnamo Oktoba 22, 2015 Bw Muturi, ambaye sasa ni Mwanasheria Mkuu (AG), aliamuru kuwa mbunge yeyote anayewasilisha hoja ya kumtimua afisini waziri, kwanza, sharti awasilishe ushahidi, kuwa njia ya hatikiapo, kuhimili tuhuma zake dhidi ya waziri huyo.

“Kabla ya mbunge yoyote kuwasilisha hoja ya kumtimua waziri afisini mwangu, lazima awasilishe hatikiapo yenye makosa anayodai waziri huyo alitenda. Nikiridhika kwamba ushahidi huo una mashiko ndipo nitatoa kibali kwa mbunge huyo kuandaa hoja yake kuambatana na hitaji la kipengele cha 156 (6) cha Katiba,” Bw Muturi akasema.

Alieleza kuwa masharti kama hayo ndio huhitajika katika nchi zingine zenye Katiba inayoipa Bunge mamlaka ya kumwondoa afisini waziri wa serikali kwa makosa mbalimbali.

“Nimetoa amri hii ili kuzuia mtindo wa baadhi ya wabunge kuwasilisha hoja za kuwaondoa mawaziri afisini kwa misingi ya sababu zisizo na mashiko yoyote,” Bw Muturi akaeleza.

Alisema hayo alipotupilia mbali hoja iliyowasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Nandi Hills, Alfred Keter ya kumwondoa afisini aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Anne Waiguru (sasa Gavana wa Kirinyaga), kwa kuhusika na sakata ya Sh790 milioni katika Shirika la Vijana kwa Huduma ya Taifa (NYS).

Kulingana na mtaaalum wa masuala ya uongozi Baraza Nyukuri, uamuzi huo wa Bw Muturi, kimsingi, umeifanya kuwa ngumu kwa waziri yeyote kuondolewa afisini kupitia bunge, ikiwa msukumo huo haujatoka kwa rais mwenyewe.

“Isitoshe, ikiwa rais na wabunge wa mrengo wake wanapinga hatua kama hiyo, itakuwa vigumu hata hoja kuidhinishwa na Spika na kujadiliwa bungeni. Kwa kuwa maspika wamekuwa wakirejelea maamuzi yaliyotolewa na watangulizi wao wanapotoa maamuzi kuhusu masuala mbalimbali yaliyowasilishwa mbele, kuna uwezekana mkubwa kwa Spika Wetang’ula atategemea uamuzi huo huo wa Muturi wa 2015 kuzima hoja ya Bw Owino na wengine wakati huu na siku zijazo,” Bw Nyukuri anaongeza.

Tayari Rais William Ruto amesema kuwa serikali haina pesa za kutimiza matakwa ya madaktari na akawaagiza warejee kazini.

Hii ina maana kuwa kiongozi wa taifa hataunga mkono njama yoyote ya kumwadhibu waziri wake yeyote kwa msingi wa mgomo huo ambao umeingia wiki yake ya nne.

Bw Owino anamlaumu Bi Nakhimicha kwa kukiuka Katiba inayotoa haki ya kila Mkenya kupata hudumu za afya kwa kufeli kutimiza matakwa ya madaktari ili wasitishe mgomo.

Aidha, aidha anamsuta Waziri huyo kwa usimamizi mbaya wa sekta ya afya na kutisha kuwapiga kalamu madaktari wanaogoma ilhali Katiba inawapa kibali cha kugoma.

Kizingiti kingine kinachomkumba Bw Owino ni kwamba tayari baadhi wabunge wa mrengo wake wa Azimio, kutoka Magharibi mwa Kenya wameapa kutounga mkono hatua yake.

Miongoni mwa wabunge hao ni Mbunge wa Butere Tindi Mwale na mwenzake wa Butere Christopher Aseka waliochaguliwa kwa tikiti ya chama cha ODM.

Huenda wakaungwa mkono na wenzake kutoka eneo hilo ambao pamoja na wale wa mrengo wa Kenya Kwanza, watavutia idadi ya wabunge ambao wanaweza kuvuruga mipango ya Bw Owino.

Hii ni kwa kumnyima idadi ya wabunge 117 (thuluthi moja ya wabunge wote 349) wanaohitaji kupitisha hoja kama hiyo, endapo itafaulu kujadiliwa bungeni.

Aidha, wadadisi wanasema kuwa itakuwa vigumu kwa hoja ya Bw Owino kuungwa mkono na chama hicho cha Chungwa ikizingatiwa kuwa kiongozi wake Raila Odinga anashirikiana na serikali ya Rais William Ruto anapoendesha kampeni ya kusaka uungwaji mkono kwa azma yake ya kutaka achaguliwe mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

“Babu Owino ametoa ilani hiyo ya kudhamini hoja ya kumwondoa afisini Waziri wa Afya Susan Nakhumicha wakati mbaya kwake. Wakati ambapo kiongozi wake, Raila anafanya kazi pamoja na Rais Ruto kumwezesha kushinda kiti cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kuelekea uchaguzi huo mwaka ujao (2024). Bila shaka hatapata uungwaji mkono kutoka kwa ODM na Raila,” anasema machanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati.

Wiki hii Rais Ruto alifanya ziara katika nchi za Afrika Magharibi za Ghana na Guinea Bissau ambapo alitumia nafasi hiyo kupigia debe Bw Odinga.

Marais Nana Akofu-Addo (Ghana) na Umaro Mokhtar (Guinea Bissau) walisema nchi zao zinaunga mkono azma ya Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Mji ambao ni ngome ya vijana wenye nywele chafu za rasta

Uhuru apiga vijembe Kenya Kwanza akiifananisha na usaliti...

T L