• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 1:01 PM
Je, unajua kwa nini bei ya kitunguu haikamatiki saa hii?

Je, unajua kwa nini bei ya kitunguu haikamatiki saa hii?

SOPHIA WANJIRU NA WANDERI KAMAU

BEI ya vitunguu imepanda mjini Nyeri kutokana na kupungua kwa mavuno ya zao hilo.

Hali hiyo imetajwa kuchangiwa na kiwango duni cha mbegu.

Kwa sasa, kilo moja ya vitunguu inauzwa kati ya Sh150 na Sh200, kutokana na uhaba wake mjini Nyeri na viungani mwake.

Bw David Marubu, ambaye ni mkulima na mfanyabiashara wa vitunguu mjini humo, aliiambia Taifa Leo kwamba mbegu zinazouzwa pia ni ghali sana.

“Nilipanda mbegu zangu kwenye nasari ila asilimia 30 yazo hazikuzaa chochote. Kabla ya kuzipeleka mahali pengine ili kuzipanda, asilimia 20 zilikauka. Mbegu tunazouziwa si za kiwango bora kwani hapo awali, asilimia 90 ya mbegu zangu zilikuwa zikimea,” akasema Bw Marubu.

Bw Marubu alitaja sababu nyingine ambayo imechangia uhaba wa zao hilo kama mvua kubwa ambayo imekuwa ikiendelea, hali ambayo imelinyima zao hilo nafasi nzuri ya kukauka. Alisema hilo limeathiri ubora wake.

“Wakati mvua inaponyesha zao hili likiwa limekomaa, huwezi kulivuna wakati halijakauka,” akasema.

Wakulima pia walilalamika kuwa ushuru mpya ambao umeanza kutozwa na serikali kwa mazao tofauti pia umewaathiri sana.

Alisema pia mbegu zilizokuwa zikiuzwa kwa Sh6,000 hapo awali zinauzwa kwa Sh10,000.

“Kwa sasa, hitaji la vitunguu liko juu sana kulitimiza. Hilo ndilo limechangia bei yake kupanda,” akasema.

Wafanyabiashara wa zao hilo walisema kuwa hapo awali, walikuwa wakinunua kilo moja ya zao hilo nchini Tanzania kwa Sh15 pekee.

“Tangu ushuru ulipoanza kutozwa kwa mazao yanayoingizwa nchini kutoka kwa mataifa jirani, yamekuwa yenye bei ghali sana. Hilo limetlazimu kunza kuyanunua humu nchini,” akasema Bw Njoroge Njogu, ambaye ni mfanyabiashara katika eneo la Asian Quarter, Kaunti ya Nyeri.

  • Tags

You can share this post!

Uchanganuzi: Ujio wa Djibouti unaweza kuharibia Raila...

Uvamizi mpya wa Al-Shabaab Milihoi wafufua kumbukumbu ya...

T L