Jenerali Ogolla, wanajeshi wengine 9 wafa katika ajali ya helikopta
KENYA inaomboleza kifo cha Mkuu wa Majeshi (KDF), Jenerali Francis Omondi Ogolla ambaye aliaga dunia Alhamisi Aprili 18, 2024 katika ajali ya helikopta eneo la Sindar kwenye mpaka wa Kaunti ya Pokot Magharibi na Elgeyo Marakwet.
Jenerali Ogolla alifariki dunia pamoja na maafisa wengi tisa waliokuwa ndani ya helikopta ya jeshi iliyokuwa na maafisa wengine 11 wa KDF ajali hiyo ilipotokea dakika chache baada ya saa tisa alasiri.
Rais William Ruto alitangaza siku tatu za kumuombeleza Jenerali Ogolla na maafisa wengine waliofariki wakiwa kazini.
“Ni siku ya huzuni. Leo nchi yetu imekumbwa na ajali mbaya iliyomuua Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Kenya, Jenerali Francis Omondi Ogolla,” Rais Ruto aliambia taifa akiandamana na makamanda wakuu wa KDF na waziri wa Ulinzi Aden Duale katika Ikulu ya Nairobi.
Maafisa hao walikuwa wakitoka katika ziara ya kikazi katika shule ya sekondari ya wavulana ya Cheptulel, Pokot Magharibi ambako walihudhuria mkutano kwa saa moja.
Rais Ruto alisema kwamba Jenerali Ogolla na maafisa wake walikuwa wametembelea wanajeshi wanaosaidia katika vita dhidi ya ujangili katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa.
Walipofika dakika chache baada ya saa saba, walipokelewa na Naibu Kamishna wa Pokot Central, Jeremiah Tumoh na mwenzake wa Chesegon Naftali Korir, machifu wa eneo hilo na maafisa wengine wa utawala.
“Kikosi cha maafisa wa KDF kiliingia moja kwa moja katika hema tulilokuwa. Miongoni mwao alikuwa Mkuu wa Majeshi Francis Ogolla ambaye aliambia wakazi kwamba shule zote zilizoathiriwa na ukosefu wa usalama zitajengwa na maafisa wa KDF,” alisema mkazi wa Cheptulel, Bw Tito Lopuriang, aliyehudhuria mkutano huo.
Alisema helikopta ya jeshi aina ya buffalo iliondoka dakika chache kabla ya saa tisa na dakika chache baadaye, wakazi wakaona moshi baada ya helikopta hiyo kuanguka eneo la Sindar upande wa Marakwet, takriban kilomita mbili kutoka Chesegon.
“Maafisa wa KDF walio eneo hilo walitumia droni kujua kilichofanyika katika eneo la mkasa,” alisema.
Bw Lopuriang alisema mwanzoni, maafisa wa usalama walifikiria ni majangili walioangusha helikopta hiyo.
“Helikopta iligonga mti na huenda ilikuwa na matatizo ya kiufundi,” alisema.
Bw Lopuriang alifichua kuwa maafisa wa KDF walifunga eneo la ajali wala hawakutaka yeyote kulikaribia.
Alisema waliookolewa walipelekwa kituo cha afya cha Kaben kwa matibabu kabla ya kusafirishwa kwa ndege.
Kamishna wa Kaunti ya Pokot Magharibi Khalif Abdullahi alithibitisha kuwa helikopta hiyo ilianguka katika mpaka wa kaunti hiyo na Elgeyo Marakwet.
Jenerali Ogolla aliteuliwa mkuu wa majeshi ya ulinzi ya Kenya mnamo Aprili 28, 2023 baada ya kustaafu kwa Jenerali Robert Kibochi mnamo Aprili 28, 2023.
Kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa majeshi, Jenerali Ogolla alikuwa naibu mkuu wa KDF.
Alisomea katika chuo cha kijeshi cha ÉcoleMilitaire de Paris, Ufaransa na katika Chuo cha Kitaifa cha Ulinzi cha Kenya.
Aidha, ana diploma katika masuala ya kimataifa na sayansi ya kijeshi kutoka Chuo Kikuu cha Egerton na digrii katika Sayansi ya Kisiasa, Utatuzi wa Mizozo na Amani na shahada ya uzamili katika Masuala ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.
Alipanda cheo katika jeshi la wanahewa hadi Meja Jenerali na kuteuliwa kamanda wa Jeshi la Angani la Kenya mnamo Julai 15, 2018, cheo alichoshikilia kwa miaka mitatu.
Akiwa Naibu Mkuu wa KDF alilaumiwa na muungano wa Kenya Kwanza ukidai alikuwa miongoni mwa wanachama wa Kamati ya Kitaifa ya Ushauri wa Usalama (NSAC) waliotembelea kituo cha kujumlisha matokeo ya kura ya urais katika ukumbi wa Bomas of Kenya kushinikiza Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutotangaza mshindi wa moja kwa moja.
Madai hayo yalikanushwa na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya na hadi kufikia kifo chake jenerali huyo hakuzungumzia suala hilo hadharani.