Jinsi hatua ya mwanafunzi kutazama ‘mwezi wa damu’ ilivyoleta zogo St George’s
MAANDALIZI ya watahiniwa wa Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) katika shule ya upili ya wasichana ya St George’s mjini Nairobi yalivurugwa baada ya shule kufungwa jana kwa muda usiojulikana.
Shule ilifungwa baada ya wanafunzi kuzua fujo kufuatia kisa ambapo inadaiwa mwalimu alimtandika mwanafunzi wa Kidato cha Pili na kumjeruhi Jumapili usiku.
Wanafunzi wengine wawili na mwalimu mmoja walijeruhiwa katika purukushani hizo.
Waliojeruhiwa walikimbizwa hospitalini, huku wanafunzi wengine wakidinda kurejea darasani au mabweni wakakesha nje hadi polisi walipoingilia kati kutuliza hali.
Jana, polisi na wasimamizi wa shule walihakikishia wazazi na wanafunzi kwamba tatizo hilo litashughulikiwa haraka ili kurejesha utulivu.
Mkuu wa Polisi (OCPD) eneo la Kilimani, Bw Patricia Yegon, aliyewasili shuleni humo akiandamana na maafisa wengine wa usalama alidinda kudokeza hatua ambayo itachukuliwa dhidi ya wahusika wa makabiliano hayo akisema uchunguzi ungali unaendeshwa.
Wazazi wamemsuta mwalimu mkuu Grace Macharia kwa kujificha na kudinda kuwahutubia.
Afisa mmoja wa usalama alieleza kuwa fujo zilizuka wakati wa masomo ya jioni mwalimu aliyekuwa kwenye zamu alipomkabiliwa mwanafunzi mmoja aliyekuwa nje wakati wenzake walikuwa darasani.
Hii ni baada ya mwalimu huyo kuwaamuru wanafunzi wengine kurejea darasani baada ya kushuhudia tukio la kipekee la Kuandamwa kwa Mwezi.
“Nilipokuwa nikiongea na wasichana hawa usiku kuanzia saa tatu, waliniambia mwenzao mmoja bado alikuwa nje wakati wengine walikuwa wamekwisha kurejea madarasani,” afisa huyo alieleza.
Alieleza kuwa mwalimu huyo alipomfikia mwanafunzi huyo na kumuuliza sababu ya yeye kusalia nje, mtafaruku ulizuka kati yao.
Wanafunzi wa Kidato cha Pili, waliokuwa darasani walishuhudia kisa hicho na wakapandwa na hasira.
Afisa huyo alisema kuwa inadaiwa kuwa mwalimu huyo alitoa kauli ya kuudhi iliyowakasirisha wanafunzi zaidi hali iliyochangia wanafunzi wote kutoka nje.
“Mwalimu huyo ambaye alikuwa katika Kidato cha 2P aliwaambia wanafunzi kwamba wakionyesha tabia za kigaidi wangeadhibitiwa vikali. Wanafunzi Waislamu waliokuwa katika darasa hilo walidhani kuwa wameitwa magaidi kwa sababu mwanafunzi aliyekuwa nje na mwalimu huyo alikuwa Mwislamu. Na hivyo, ndivyo shida ilianza,” akasema.
Suala hilo lilivumishwa na wanafunzi wa vidato vingine wakajitokeza, wakiwashambulia walimu.
Kulingana na wanafunzi, wenzao wawili walijeruhiwa katika makabiliano hayo na walimu, mmoja akiwa mwanafunzi wa Kidato cha Tatu.
Mkuu wa Polisi wa eneo la Kilimani (OCPD) Patricia Yegon aliyewasili shuleni humo akiandamana na maafisa wengine wa usalama alidinda kuseama hatua ambayo itachukuliwa dhidi ya wahusika katika makabiliano hayo akisema uchunguzi ungali unaendeshwa kuhusu kisa hicho.
Baadhi ya wazazi waliofika shuleni humo walidai kuwa usimamizi ulidinda kushughulikia suala hilo kwa haraka na wakataka waruhusiwe kuenda nyumbani na watoto wao.
Baadhi ya wazazi waliofika shuleni humo walimsuta mwalimu mkuu Grace Macharia kwa kujificha na kudinda kuwahutubia.