• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Jinsi mshukiwa wa ulanguzi mihadarati kupitia wanafunzi wa kike alivyonyakwa

Jinsi mshukiwa wa ulanguzi mihadarati kupitia wanafunzi wa kike alivyonyakwa

NA WINNIE ATIENO

MAAFISA kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) wamemkamata mwanamume anayeshukiwa kuwa mhusika mkuu wa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Maafisa hao wanaoshika doria katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi, Mombasa, walimkamata Bw Salim Kalinga Mwinyi kuhusiana na madai ya ulanguzi wa mihadarati.

Maafisa hao pia walivamia nyumba ya mshukiwa huyo mtaa wa Magogoni, eneo la Kisauni, na kupata kilo moja ya heroini, bangi, mizani na Sh1.7 milioni pesa taslimu.

Polisi walisema fedha hizo ambazo inashukiwa kuwa zilitokana na biashara hiyo haramu, zilipatikana kwenye nyumba ya mshukiwa ambapo alikuwa akiendeleza shughuli hiyo ya ulanguzi pamoja na mkewe.

“Mnamo saa tisa usiku, maafisa wa DCI kutoka kitengo cha doria katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege ya Moi walipata habari kuhusu mshukiwa Salim Kalinga Mwinyi na kuvamia nyumba yake na kupata vitu hivyo,” taarifa kutoka idara ya polisi ilisema.

Makachero hao, walisema mshukiwa huyo anayehudumu eneo la Pwani amekuwa akishukiwa kwa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Kulingana na maafisa hao, mshukiwa huyo alikuwa mpinzani wa kibiashara wa marehemu Swaleh Yusuf Ahmed, maarufu Kendereni.

Bw Ahmed alipatikana ameuawa wiki mbili zilizopita katika kisa ambacho maafisa wa polisi walitaja kuwa uhasimu wa kibiashara.

Idara ya Usalama ikiongozwa na Waziri wa Usalama wa Usalama, Prof Kithure Kindiki, ilipinga madai ya kuhusika na mauaji hayo wakiitaka familia yake kuwasilisha ripoti hiyo kwa uchunguzi.

“Kwenye biashara hiyo ya ulanguzi wa dawa za kulevya na usambazaji wa bidhaa hiyo, wawili hao walikuwa mahasimu wakubwa hasa katika eneo la Magodoroni na Arusini eneo la Kisauni,” ripoti ya usalama ilisema.

Maafisa wa polisi walidai kuwa Bw Mwinyi alikuwa akitumia wanafunzi wa shule wa kike hasawa familia yake, kusambaza mihadarati.

Polisi pia walisema kuwa wake wawili wa mshukiwa, wamewahi kukamatwa na kesi dhidi yao bado zinaendelea mahakakamani.

Mshukiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu, Aprili 15, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Athari za vita vya Israel-Iran kwa Kenya

Janga jipya la mafuriko

T L