Jinsi mwanamume alifika lango la Ikulu, akapiga stori na GSU kabla ya kumuua
JAPO Ikulu ni kati ya maeneo yenye ulinzi mkali zaidi nchini, jana taifa lilijipata katika mshangao mkubwa baada ya afisa wa polisi wa GSU kudungwa kwa mshale nje ya lango la kuingia katika makazi hayo ya hadhi hadi akafa.
Msemaji wa Polisi Michael Nyaga kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, alithibitisha mauaji hayo ambapo afisa wa polisi wa cheo cha Konstebo Ramadhan Mattanka alidungwa kwa mshale na mwanamume kwa jina Kithuka Kimunyi.
Tukio hilo lilijiri jana saa mbili na dakika 10 asubuhi karibu na Lango D nje ya Ikulu.
Kimunyi mwenye umri wa miaka 56, alikuwa amebeba upinde na mishale kabla ya kuwakaribia maafisa wa polisi ambao kwa kawaida hulinda eneo hilo.
“Licha ya kuambiwa ajisalimishe aliendelea kuwakaribia maafisa hao. Alimkaribia Ramadhan Mattanka kisha akamlenga na kumdunga kwa mshale kwenye ubavu wake wa kushoto,” ikasema taarifa ya Bw Nyaga.
“Maafisa wa GSU ambao walikuwa kwenye zamu waliharakisha na kumkamata mwanaume huyo,” ikaongeza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilifafanua kuwa Mattanka alikimbizwa hadi Hospitali ya Kenyatta ambako aliaga dunia akiendelea kupokea matibabu. Mwili wake ulihamishwa hadi hifadhi ya maiti ya hospitali hiyo ili ufanyiwe upasuaji wa maiti.
“Tume ya Huduma za Polisi inalaani mauaji haya na wakati huo huo inawapongeza maafisa waliowajibika kuhakikisha hakuna majeraha zaidi. Uchunguzi bado unaendelea,” ikasema taarifa ya Bw Nyaga.
Msemaji huyo wa polisi alisema bado uchunguzi unaendelea kuhusu tukio hilo na kuwa jamaa wa polisi aliyeuawa wamepewa taarifa kuhusu mauti yake.
“Tunasimama nao wakati huu mgumu. Tunatuma rambirambi kwa familia, marafiki na jamaa wa marehemu afisa wa cheo cha konstebo, Ramadhan Mattanka,” ikasema taarifa.
Mitandaoni video ilisambaa ikionyesha Kimunyi aliyevalia fulana nyeupe akiwa katika gari la polisi na pingu mikononi.
Akiwa amekaza macho na kuonekana kutokuwa na wasiwasi wowote, Kimunyi ambaye alikuwa ameegemeza kichwa kwenye gurudumu la gari aliwauliza polisi kuwa amefanya nini?
“Hujui chenye umefanya, utajua tu,” polisi aliyekuwa naye garini alisikika akimwambia.
Polisi nao waliwajibu wanahabari kuwa Kimunyi alikuwa akipelekwa hospitalini lakini hawakufafanua iwapo alikuwa anapelekwa kupimwa utimamu wake.
Katika video ya pili, Kimunyi alionekana akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi kwenye gari lao akipelekwa hospitalini.
Wachanguzi wanataka kubaini iwapo Mattanka au hata maafisa wanaofanya kazi naye walikuwa na uhusiano na Kimunyi kwa sababu si rahisi kwa raia yeyote wa kawaida kuruhusiwa kuingia ikuluni.
Kanda za CCTV zilimwonyesha Mattanka akiwa ameanguka chini kama amelemewa na uchungu huku wenzake wakikimbia kuyanusuru maisha yake lakini wakawa wamechelewa.
Mkuu wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya Uhalifu (DCIO) wa Kilimani, Mahat Hassan alisema kuwa Kimunyi alikuwa akitembea karibu na ikulu ndipo Mattanka akamkaribia.
Ripoti katika kituo cha polisi cha Kilimani nayo ilisema kuwa Kimunyi aliwaendea maafisa wanaolinda lango la kuingia ikulu waliokuwa wakiyakagua magari mawili.
“Alitoa mshale na kumdunga Ramadhan Khamisi Mattanka kwenye kifua cha kushoto na kumwacha akitokwa na damu nyingi. Alikamatwa naye afisa huyo akafikishwa hadi hospitali ya Kenyatta ambako aliaga dunia eneo la kuwapokea wagonjwa mahututi,” ikasema ripoti ya afisa wa GSU, Daniel Kemboi.
Familia ya marehemu afisa huyo wa GSU jana iliitikia ombi la polisi kuwa waahirishe mazishi yake.
Hii ni kwa sababu kulingana na imani ya Kiislamu, familia ya Mattanka ilitaka azikwe kabla ya jua kutua jana Jumatatu.
Hata hivyo, polisi waliomba mazishi hayo yaahirishwe ili mwili wake ufanyiwe uchunguzi wa maiti leo Jumanne.