Habari za Kitaifa

Jinsi sera ya Rais Ruto inavyozuia raia wa kigeni kuja Kenya

Na  CONSTANT MUNDA November 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERA ya utawala ya Rais William Ruto inayowahitaji  raia wa nchi za kigeni kujiandikisha mtandaoni siku tatu kabla ya kusafiri kuja Kenya imeifanya Kenya kuwa miongoni mwa nchi ngumu zaidi kutembelea barani 2024, ripoti mpya inaonyesha.

Kenya imeshuka nafasi 17 katika orodha ya nchi rahisi kutembelea hadi nambari 46 kati ya nchi 54 barani Afrika, kwa mujibu wa Ripoti ya Uwazi ya Visa ya Afrika 2024 ambayo hupima jinsi ilivyo rahisi kwa Waafrika kuingia katika mojawapo ya nchi za bara hili.

Kenya imeshuka kutoka nambari 29 mwaka jana, na kuifanya kuwa na alama mbaya zaidi tangu 2016,  Muungano wa Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) zilipoanza kufanya utafiti huo kila mwaka.

Kenya imepoteza nafasi yake ya kuwa miongoni mwa nchi zinazokaribisha watu wengi zaidi barani humu, baada ya kuorodheshwa nambari tisa mwaka wa 2018 ilipofuta mahitaji ya viza kwa wageni kutoka Afrika.

Kutekelezwa kwa mfumo wa Kielektroniki wa Kuthibitisha Usafiri (eTA), ulioanza Januari 5 kumeathiri Kenya.

Chini ya eTA, wageni wanahitajika kutuma maombi ya kuingia Kenya saa 72 kabla ya kuwasili na walipe $30 (takriban Sh3,900), hali ambayo wachambuzi wanasisitiza kuwa ni visa kwa jina tofauti.

“Kenya sasa inahitaji eTA kabla ya raia wa kigeni kuzuru nchi hiyo isipokuwa kwa raia wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hizi ni Burundi, DRC, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda, huku wakati wa kuandika ripoti, Somalia haikuwa imejumuishwa katika orodha hii ya nchi zilizopewa msamaha,” AfDB iliandika katika  ripoti ya Uwazi kuhusu Viza Afrika, 2024.

Baada ya malalamishi mapema mwakani Idara ya Uhamiaji na Huduma kwa Raia iliwasamehe raia wa Ethiopia, Afrika Kusini, Ngazija, Congo-Brazzaville, Eritrea, Msumbiji na San Marino kulipa ada hizo wanapotuma maombi ya kutembelea Kenya kupitia eTA.