Habari za Kitaifa

Jinsi Sh5b zilivyopotea kwa viwanda vilivyokuwa vianzishwe na Waziri Moses Kuria

Na MOSES NYAMORI December 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

YALIVUMISHWA na utawala wa Rais William Ruto kama suluhu ya ukosefu mkubwa wa ajira nchini na kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa mashinani.

Wakiyataja kuwa miongoni mwa miradi mikuu ya Kenya Kwanza, maafisa wakuu wa serikali wakiongozwa na aliyekuwa Waziri wa Biashara, Moses Kuria, walianza kazi kwa kasi mnamo 2023, wakizuru kaunti mbalimbali kuzindua ujenzi wa maeneo ya viwanda kwa shamrashamra, sherehe na matangazo ya moja kwa moja kupitia runinga.

Hata hivyo, kulingana na ripoti ya Ofisi ya Bajeti ya Bunge (PBO), karibu miaka mitatu baadaye, hakuna hata eneo moja la viwanda katika Kaunti lililokamilika.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa, kaunti 13 bado hazijaanza miradi hiyo kabisa. Kaunti hizo ni Bomet, Elgeyo/Marakwet, Isiolo, Kisumu, Lamu, Mandera, Makueni, Nairobi, Samburu, Taita Taveta, Tharaka Nithi, Turkana na Pokot Magharibi.

Kiwango cha utekelezaji katika kaunti nyingine 16 ni asilimia 30 au chini. Hizi ni Narok (asilimia 10), Murang’a (10), Mombasa (10), Vihiga (15), Kajiado (16), Nyandarua (17), Laikipia (20), Kakamega (22), Siaya (23), Nyeri (25), Trans Nzoia (25), Kilifi (30), Baringo (30), Nyamira (30), Nandi (30) na Nakuru (30).

Ni kaunti 14 pekee ambako utekelezaji ni zaidi ya asilimia 50.

Kila kaunti ilitakiwa kutenga Sh250 milioni huku serikali ya kitaifa kupitia Idara ya Viwanda pia ikitenga Sh250 milioni kwa kila kaunti. Hii ina maana kuwa kila ngazi ya serikali ilipaswa kutenga Sh11.5 bilioni zote kuwa Sh 23.5 bilioni.

Kwa mujibu wa ripoti ya PBO yenye kichwa ‘Devolution Budget Watch 2025,’ ni kaunti 10 pekee zilizopokea mchango kamili wa Sh250 milioni kutoka kwa serikali ya kitaifa ikiwa ni jumla ya Sh2.5 bilioni.

Kwa kuzingatia makubaliano ya kuchangia kiasi sawa, kaunti hizo pia zilipaswa kutenga Sh2.5 bilioni. Hii inamaanisha kuwa Sh 5 bilioni tayari zimetumika katika miradi iliyokwama.

Ripoti inaonyesha kuwa, katika mwaka wa kifedha wa 2025/26, serikali itatoa fedha zaidi, Sh4.45 bilioni ambazo zimetengewa kaunti nyingine 24.

Baadhi ya kaunti zitapokea kiasi kamili cha Sh250 milioni huku zingine zikipata kiasi cha chini hadi Sh 50 milioni.

PBO ni afisi huru ya kitaalamu ya Bunge, iliyo na jukumu la kutoa huduma za kitaalamu kuhusu bajeti, fedha na taarifa za kiuchumi kwa kamati za Bunge.

Mnamo Agosti 2023, Bw Kuria aliahidi kuwa kaunti zote zingekuwa na maeneo ya viwanda ndani ya miezi 12.

Hata hivyo, mnamo Oktoba 2023, alihamishwa kutoka wizara hiyo Oktoba 2023 na kupewa Wizara ya Utumishi wa Umma katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Baadaye alivuliwa uwaziri rais alipovunja baraza la mawaziri kufuatia maandamano yaliyoongozwa na vijana Juni 2024.

Katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Kuria alitaja utekelezaji wa mradi huo kama “ndoto iliyopotea” na kuwataka wanaohusika wachukue hatua kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.

Akirejelea maono ya Rais Ruto ya kufanya Kenya kuwa taifa lililostawi duniani, Bw Kuria alisema kuwa maeneo hayo ya viwanda yangekuwa njia ya haraka zaidi ya Kenya kufanikiwa kama Singapore.

Alisema lengo lilikuwa kuunda nafasi za ajira kwa maelfu ya vijana wasio na ajira na pia kupunguza idadi ya watu wanaohama kutoka mashambani kwenda mijini.

“Niliwauzia magavana maono haya nikiwa Naivasha, na kila kitu kilikuwa kinaenda vizuri. Kufikia wakati nilipohamishwa, nilikuwa nimezindua maeneo ya viwanda katika kaunti 16. Kaunti zilikuwa na ari kubwa na zilikuwa zinashindana kutenga fedha,” alisema Bw Kuria.

“Kwa sasa, tungekuwa na mamia ya vijana wakifanya kazi katika maeneo hayo. Wito wangu ni kwa walio na jukumu, wachukue hatua, kwa sababu hii ndiyo Singapore ya kweli. Nililenga kuwa na viwanda katika kaunti, lakini maono hayo yalipotea kabisa.”

Katika kaunti 10 zilizopokea mchango kamili kutoka kwa serikali ya kitaifa, ripoti inaonyesha kuwa hakuna hata moja iliyokamilisha ujenzi.

Meru ina kiwango cha utekelezaji cha asilimia 92, Embu (83), Kirinyaga (81), Migori (80), Garissa (79), Busia (70), Machakos (61), Uasin Gishu (55), Bungoma (54) na Homa Bay (47).

Ripoti inaeleza kuwa mpango ni kuwezesha kukamilika kwa miradi hiyo katika kaunti 24 nyingine kwa kutoa sehemu ya mgao wa Sh 250 milioni kutoka kwa serikali ya kitaifa katika mwaka wa kifedha wa 2025/26.