• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Jinsi video ya ubakaji ya genge la wanaume saba ilifichuka

Jinsi video ya ubakaji ya genge la wanaume saba ilifichuka

Na VITALIS KIMUTAI

VIDEO inayosawiri kitendo cha ubakaji inayosambaa katika mitandao ya kijamii ilinaswa miezi minne iliyopita na kutolewa na mshukiwa aliyetoroka baada ya kutekeleza uhalifu mwingine.

Mshukiwa huyo, aliyetorokea Nairobi baada ya kugundua kuwa polisi walikuwa wakimwandama, alitoa video hiyo kama njia ya kulipiza kisasi dhidi ya washirika wake, kulingana na uchunguzi wa polisi.

Hata hivyo, haijulikani ikiwa washukiwa katika video hiyo ni wahusika katika uhalifu ambao mshukiwa huyo anasakwa kuhusu.

Hadi tulipokuwa tukienda mitamboni, mwathiriwa aliyeonekana kubakwa na wanaume hao, hakuwa amepatikana na polisi ili aandikishe taarifa.

Kisa hicho kilitendeka katika eneo la Chebanyiny, kata ya Olbutyo, wadi ya Kongasis, Kaunti ya Bomet.

Polisi wanasema washukiwa hao ambao walikuwa katika starehe za kunywa pombe iliyoanza katika kituo cha kibiashara cha Kapkwen, walikuwa wametumia dawa za kuongeza nguvu za ngono.

Kamanda wa Polisi Kaunti ya Bomet, Bw Robinson Ndiwa, alithibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao saba.

“Wawili kati yao walitambuliwa kama; Anderson Mutai, 38, na Weldon Sigei, 21,” Bw Ndiwa akasema.

Bw Ndiwa alisema kisa hicho hakikuripotiwa kilipotendeka.

“Lakini uhalifu huu ulikuwa mbaya zaidi na ulipaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria,” akaeleza. Polisi wanamsaka mwanamke mwathiriwa ili aandikishe taarifa kuhusiana na unyama aliotendewa na wanaume hao saba.

Uchunguzi wa awali ulioendeshwa na polisi ulionyesha kuwa mhasiriwa alishawishiwa, na mmoja wa washukiwa, kuingia chumbani humo baada ya wao kubugia pombe usiku.

Baadaye, mwanamume huyo aliwaita marafiki zake na wakatenda uhalifu huo huku akirekodi katika simu yake ya rununu.

Nyuso za baadhi ya wanachama wa genge hilo zinaonekana vizuri katika kanda hiyo ya video, ilhali nyuso za wengine hazionekani vizuri.

Bw Edwin Barusei, ambaye ni chifu wa kata ya Kongasis, alithibitisha kuwa aliyenasa video hiyo hajapatikana na polisi wanamsaka pamoja na washukiwa wengine.

“Ni kweli kwamba mshukiwa huyo, anayesakwa kwa kosa lingine, ametoroka na inaaminika alitoa video hiyo ili kuwafichua wenzake wahusika katika kitendo hicho cha unyama kilichoshtua wengi. Inaonekana kuwa hakutaka kuandamwa pekee yake kwa uhalifu ule mwingine,” Bw Barusei akasema.

Inasemekana kuwa mshukiwa mmoja alishangaa kugundua kuwa alishiriki katika uhalifu huo akiwa katika hali ya ulevi baada ya kutumia pombe na dawa hizo.

Aidha, inadaiwa kuwa hakufahamu kuwa alikuwa akitenda uhalifu mbaya zaidi wa ubakaji wa pamoja.

Wazee, viongozi, makasisi, wanawake na watetezi wa haki za kibinadamu wamelaani kisa hicho na kutaka washukiwa waadhibiwe vikali.

“Kwa vyovyote vile, waliomtendea mwanamke huyu unyama wa aina hii sharti waadhibiwe vikali ili iwe funzo kwa watu wengine wenye nia ya kutenda uhali wa aina hiyo,” akasema Bi Irene Cherotich Terer, ambaye ni kiongozi wa vijana na mfanyabiashara.

  • Tags

You can share this post!

Lango maalum la kuingia mji wa Lamu ambalo usipolipitia...

Mpenzi wa zamani wa Ruben Dias amtema kiungo wa Sheffield...

T L