John Matara ashtakiwa kwa wizi wa mabavu, ubakaji
NA RICHARD MUNGUTI
MSANII John Matara, ambaye alishtakiwa kwa mauaji ya Starlet Wahu, amefikishwa kortini tena kwa mashtaka ya wizi wa mabavu na ubakaji.
Bw Matara alishtakiwa mbele ya Hhakimu Mwandamizi Charles Mwaniki katika Mahakama ya Ruiru, Kaunti ya Kiambu.
Bw Matara alikana alimnyang’anya kimabavu mwanamke Sh48,300 pamoja na simu mbili za kiunga mbali za thamani ya Sh40,000 na vilevile kitambulisho, kadi ya benki na pasipoti katika mtaa wa Kahawa Wendani mnamo Mei 16, 2023.
Bw Matara alikana pia siku hiyo hiyo alimlawiti na tena kumbaka mwanamke aliyempora kimabavu.
Wakili Samuel Ayora anayemtetea Bw Matara aliomba mahakama imwachilie kwa dhamana.
Mbali na ombi hilo la dhamana, Bw Ayora aliomba mahakama iamuru mshtakiwa apelekwe hospitali akidai “aliumizwa na polisi kwa kuvurutwa nyeti zake.”
Wakili huyo alieleza mahakama mshtakiwa anaumia na hata hawezi kutembea vizuri.
Mahakama iliombwa iamuru ripoti ya daktari atakayempima na kumtibu mshtakiwa iwasilishwe kortini.
Na wakati huo huo, kiongozi wa mashtaka aliomba sampuli zitolewe kwa mshtakiwa kufanyiwa vipimo vya DNA kutumika kama ushahidi katika kesi inayomkabili mshtakiwa.
Pia kiongozi huyo wa mashtaka alipinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana akisema “atatoroka na mahala anapoishi hapajulikani.”
Hakimu aliombwa asikubali madai kwamba nyeti za mshtakiwa ziliumizwa kwa kuvurutwa na polisi akipelekwa mahakama ya Ruiru kujibu shtaka.
Hakimu aliombwa aamuru mshtakiwa apige ripoti katika kituo cha polisi ili madai hayo yachunguzwe na ripoti kutolewa.
Mahakama iliamuru mshtakiwa apelekwe hospitalini kutibiwa na ripoti kuwasilishwa kortini.
Pia alitakiwa awasilishe malalamishi yake kuwa alitendewa unyama na polisi kwa polisi ili yachunguzwe.
Mshtakiwa aliagizwa asalie katika gereza la Industrial Area hadi Machi 8, 2024, ombi lake la dhamana litakapotolewa.
Bw Matara alishtakiwa kumuua Starlet katika mtaa wa South B, Nairobi.
Soma Pia: Uchunguzi kuhusu mshukiwa wa mauaji ya Starlet Wahu wakamilika