Jowie awasilisha notisi ya kukata rufaa
NA RICHARD MUNGUTI
JOSEPH Irungu almaarufu Jowie, aliyehukumiwa kifo kwa kosa la kumuua Monicah Kimani, amewasilisha notisi ya kukata rufaa.
Amepanga kuwasilisha rufaa dhidi ya kupatikana na hatia ya mauaji na pia hukumu iliyotolewa.
“Mahakama ya Rufaa inafahamishwa kwamba Joseph Kuria Irungu almaarufu Jowie, anapinga uamuzi wa Jaji Grace Nzioka ambaye akiwa katika mahakama ya Milimani, Nairobi mnamo Februari 9, 2024, ambapo alimpata mkata rufaa na hatia ya mauaji na akampokeza adhabu ya kifo mnamo Machi 13, 2024,” notisi ikasema.
Adhabu ilitolewa na jaji Nzioka mnamo Machi 13, 2024.
Akipokezwa adhabu hiyo, Jowie aliinama baada ya kusikia jaji Nzioka akiliita jina lake kama mwalimu anayefundisha wanafunzi kutamka herufi kwa kukawia kutamka neno lililofuata.
Kimya kilitanda ndani ya korti.
Bi Nzioka aliita jina la mfungwa Joseph Kuria Irungu kwa ufasaha kisha akaangusha kombora lililokuwa limesubiriwa.
“Umehukumiwa kunyongwa kwa kumuua Monicah Kimani kwa mujibu wa sheria za Kenya,” akasema Bi Nzioka.
Baada ya tamko hilo, kimya kingine kilitanda kortini kana kwamba mahakama ilikuwa mahame.
Ni wakati huo maafisa wa idara ya magereza wapatao saba walisimama huku kamanda wao akielekea kizimbani alikokuwa Jowie na kumtia pingu kisha askari jela hao saba wakamtoa Jowie kizimbani na kumpitishia veranda kumpeleka gereza kuu la Kamiti kusubiri siku 14 akate rufaa.
Baada ya kuhukumiwa, Jowie alimtimua kazi wakili Hassan Nandwa na kumteua wakili Andrew Muge kumtetea na kukata rufaa.
Akihojiwa na Taifa Leo, wakili Muge alisema ataangazia katika ushahidi ambao haukuguswa na Bi Nzioka ambao ungemwondolea lawama mteja wake ambaye ni Jowie.
Kesi hii ya mauaji ya Monicah ambaye alikuwa na umri wa miaka 28 alipokatwa koo, ilianza kusikilizwa na Jaji James Wakiaga mwaka 2018 na kumaliziwa na Bi Nzioka mnamo Machi 13, 2024.
Sasa kilichobaki ni rufaa ya Jowie kama alivyoweka kwa notisi yake kwa mahakama Ijumaa.