Habari za Kitaifa

JSC sasa yamkingia Mwilu dhidi ya kuandamwa na Gachagua

Na JOSEPH WANGUI August 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) imekataa ombi lililowasilishwa kwake la kutaka kumwondoa Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu afisini kwa madai ya utovu wa nidhamu kwa kuteua, kinyume cha sheria, majaji walioshughulikia kesi ya kumuondoa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Ombi hilo, lililowasilishwa na Belinda Egesa, pia lilidai kuwa Bi Mwilu alionyesha kukosa uwezo wa kutekeleza majukumu yake mbali na kukiuka Katiba kwa kutumia mamlaka ya Jaji Mkuu Martha Koome bila idhini.

Hata hivyo, JSC ilisema kuwa ombi hilo halikufikia kiwango kinachohitajika kwa mujibu wa Kifungu cha 168 cha Katiba, ambacho kinaainisha msingi wa kumwondoa jaji kazini.

Pia, tume hiyo haikupata ushahidi kuwa Bi Mwilu alitenda hilo kwa nia mbaya.

Kifungu hicho kinasema jaji anaweza kuondolewa kazini ikiwa hawezi kutekeleza majukumu yake kwa sababu ya matatizo ya kiakili au kimwili, kufilisika, utovu wa nidhamu, au kuvunja sheria au maadili ya mahakama.

JSC ilisema kuwa japo Mahakama ya Rufaa ilibaini kuwa Bi Mwilu alikiuka mamlaka kwa kuteua majaji, hatua hiyo ilichukuliwa kwa nia njema, kutokana na ukosefu wa uwazi wa kikatiba kuhusu nani anapaswa kutekeleza majukumu ya Jaji Mkuu anapokuwa hayupo.

“Ingawa Mahakama ya Rufaa ilibaini kuwa Naibu Jaji Mkuu alivuka mipaka ya mamlaka yake, tume ilizingatia kuwa hatua hizo zilichukuliwa kwa nia njema, kwa kuzingatia utata wa kikatiba na wa kimfumo uliokuwepo wakati huo kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Jaji Mkuu,” alisema Katibu wa JSC, Wilfridah Mokaya.

Tume hiyo ilisema kuwa wakati Bi Mwilu alipowateua majaji Erick Ogola, Anthony Mrima na Dkt Freda Mugambi kusikiliza kesi hiyo ya kumng’oa Gachagua, kulikuwa na suitafahamu ya kisheria kuhusu majukumu yake.

Hali hiyo ilithibitishwa na Mahakama ya Rufaa katika uamuzi wa Mei 9, 2025.

Hivyo basi, JSC iliamua kuwa hakukuwa na ushahidi wa nia mbaya au utovu wa nidhamu dhidi ya Naibu Jaji Mkuu, na kwamba hatua zake zilichochewa na suitafahamu halali ya kisheria, na si kwa makusudi ya kuvuruga sheria.

Bi Egesa alikuwa amedai kuwa Bi Mwilu alivunja Katiba na kanuni za Maadili ya Mahakama za mwaka wa 2020 kwa kushindwa kuelewa Kifungu cha 165(4) cha Katiba kinachohusu mamlaka ya Jaji Mkuu wa kuteua jopo la majaji kwa kesi zinazohitaji tafsiri kubwa ya kisheria.

Ombi hilo lilitokana na uamuzi wa Mahakama ya Rufaa kwamba uteuzi wa majaji Ogola, Mrima na Mugambi kuisikiliza kesi ya wakazi wa Kaunti ya Kirinyaga waliokuwa wakipinga kuapishwa kwa Prof Kithure Kindiki kama Naibu wa Rais badala ya Bw Gachagua, haukuwa halali kisheria.

Mahakama ya Rufaa ilibaini kuwa jopo hilo liliteuliwa kinyume cha sheria, kwani Naibu Jaji Mkuu hakuwa na mamlaka ya kutumia madaraka ya Jaji Mkuu.

Kwa msingi huo, Bi Egesa alitaka JSC ichunguze mwenendo wa Bi Mwilu na kuwasilisha pendekezo kwa Rais kumwondoa kazini kwa sababu za utovu wa nidhamu, kutoheshimu Katiba, na kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

“Matokeo ya vitendo kinyume cha Katiba ya Naibu Jaji Mkuu, kwa kuteua jopo la majaji kwa njia isiyofaa, yalipelekea kuondolewa kwa maagizo ya muda ya Mahakama ya Kerugoya, hivyo kuruhusu Profesa Kindiki kuapishwa kuwa Naibu Rais. Tukio hilo haliwezi kubatilishwa sasa,” walieleza mawakili wa Bi Egesa.

Walidai kuwa Bi Mwilu alivunja Katiba kwa kutumia mamlaka ambayo kikatiba ni ya Jaji Mkuu tu, hivyo hatua yake ya kuteua majaji mnamo Oktoba 18, 2024, ilikuwa nje ya uwezo wake kisheria.