JSC yaorodhesha watu 100 kuwania nafasi 20 za majaji wa Mahakama Kuu
NA WANDERI KAMAU
TUME ya Huduma za Mahakama (JSC) imewaorodhesha watu 100 watakaowania nafasi za majaji wa Mahakama Kuu.
Tume hiyo ilikuwa imetangaza nafasi 20 za majaji wa Mahakama Kuu kwenye tangazo lililowekwa kwenye gazeti rasmi la serikali mnamo Oktoba 13, 2023.
Kwenye taarifa Ijumaa, Jaji Mkuu Martha Koome alisema kuwa kufikia wakati wa kufunga muda wa kupokea maombi ya nafasi hizo hapo Novemba 3, 2023, walikuwa wamepokea maombi 305.
“Baada ya kutathmini na kuzingatia maombi yote yaliyowasilishwa kwetu, tumewaorodhesha watu 100, kwani maombi yao yalilingana na mahitaji yaliyowekwa kwenye tangazo,” akasema Bi Koome.
Watu hao watafanyiwa usaili kati ya Aprili 3 hadi Aprili 30, 2024, katika jumba la CBK Pension Towers, Orofa ya 13, Harambee Avenue jijini Nairobi.
Watu waliotuma maombi wanaweza kupata orodha ya wale watakaohojiwa na tarehe maalum kwenye tovuti ya tume hiyo.
Tume pia imeualika umma kutoa maelezo yoyote muhimu kuhusu watu walioorodheshwa kufikia Machi 21, 2024, saa 11 jioni.
Wale watakaoteuliwa watahudumu kama Majaji wa Mahakama Kuu kwa kuendesha na kusimamia kesi zinazohusu masuala uhalifu na jinai.
Kwa mtu kuteuliwa katika nafasi hiyo, lazima awe na shahada ya sheria kutoka chuo kinachotambuliwa, awe wakili wa Mahakama Kuu ya Kenya au awe na vigezo kama hivyo kutoka nchi inayoendesha mfumo sawa wa kisheria na Kenya.
Pia, wanafaa wawe na tajriba ya miaka kumi kama jaji wa mahakama wa ngazi ya juu au hakimu aliyehitimu.
Zaidi ya hayo, lazima wawe na tajriba ya angaa miaka kumi kama wasomi wa masuala ya kisheria au majukwaa mengine ya kisheria.
Vile vile, lazima wawe wametimiza mahitaji na vigezo vya uwajibikaji, kulingana na Sura ya Sita ya Katiba kuhusu Uongozi na Maadili.