Habari za Kitaifa

Kaa chonjo: Kenya kukumbwa na mwezi wa damu angani

Na ELVIS ONDIEKI September 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kenya inatarajiwa kushuhudia tukio la nadra la anga linalojulikana kama “mwezi wa damu” leo jioni, ambalo litadumu kwa dakika 82. Wakati huo huo, serikali itaitumia fursa hiyo kuzindua bidhaa mpya ya utalii.

Wakati baadhi ya sehemu za dunia kama Amerika zitakuwa zikifurahia jua la adhuhuri, upande wao wa dunia utakuwa ukizuia mwanga wa jua kufikia mwezi. Kivuli cha Dunia kitaonekana kwenye mwezi, na katika maeneo ya Afrika, Asia, Australia na sehemu za Ulaya, hali hiyo itafanya mwezi kuonekana kama una damu.

Tukio hili linatokana na kile kinachojulikana kama kupatwa kamili kwa mwezi ambapo Dunia hujipanga kati ya jua na mwezi na hivyo kuzuia mwanga wa jua kufikia mwezi. Hata hivyo, Dunia haizuii mwanga wote; hewa ya Dunia huchuja mwanga na kuruhusu miale nyekundu kupenya na kufikia mwezi. Miale hiyo nyekundu ndiyo inayopatia mwezi mwonekano wake wa kutisha wa damu, licha ya kuwa umbali wa kilomita 384,400 kutoka Dunia.

Kwa mujibu wa Shirika la Kitaifa la Anga na Safari za Ndege za Anga la Amerika (NASA), ikiwa utakosa tukio hilo leo  nafasi nyingine ya kulishuhudia itakuja tena Desemba 31 2028. Kupatwa kamili kwa mwezi kulikoshuhudiwa mara ya mwisho nchini Kenya ilikuwa Mei 2022. Tukio linalofuata litafanyika Machi 3, 2026, lakini halitaonekana kutoka Kenya.

Shirika la Anga la Kenya (KSA) limesema kupatwa kamili kwa mwezi kutaanza saa mbili na nusu usiku na kuisha saa tatu na dakika 53 usiku. Hata hivyo, kati ya saa kumi na mbili na dakika 28 jioni na saa tano na dakika 55 usiku, mwezi utakuwa wa kawaida kwani utakuwa unaingia na kutoka kwenye kivuli cha Dunia, hali itakayoufanya ubadilishe rangi kwa hatua hadi kufikia rangi nyekundu zaidi.

Katika hatua ya kuvutia watalii, Bodi ya Utalii ya Kenya (KTB) imepanga kutumia tukio hili la mwezi wa damu kuzindua rasmi bidhaa mpya ya utalii inayoitwa “astro-tourism”, au utalii wa angani. Hii inalenga kuvutia watu wanaozunguka dunia kushuhudia matukio ya nadra ya angani.

“Astro-tourism ni soko jipya linalochipuka linalochanganya kutazama nyota, elimu ya anga na uzoefu wa kuona anga usiku bila uchafuzi wa mwanga,” ilisema taarifa kutoka kwa Bodi ya Utalii ya Kenya.