Wivu utawaua bure, Passaris haendi mahali, viongozi wa kike Nairobi waapa
BAADHI ya viongozi wa kike mashinani kutoka Kaunti ya Nairobi wamejitokeza na kumtetea Mbunge Mwakilishi wa Kike Esther Passaris ambaye anakodolewa macho na kungátuliwa kutokana na shinikizo za wapigakura.
Kwenye kikao na wanahabari Jumanne, viongozi hao walisema Bi Passaris anastahili kupewa muda akamilishe muhula wake.
Diwani Maalum Cecilia Wairimu aliwaongoza viongozi hao wa mashinani kutangaza kuwa juhudi ambazo zimeanza kumng’oa Bi Passaris ni kama kufungua uwanja wa vita dhidi ya viongozi wanawake nchini na zinaongozwa na wivu.
Alisema Bi Passaris analengwa tu kwa sababu anaunga mkono utawala wa Rais William Ruto ambao unachukiwa na wanaotaka kung’atua
“Esther Passaris ni mwanamke kama sisi na wamruhusu amalize muhula wake. Wasubiri hadi 2027 ndipo wamngóe au wamrejeshe, kama wanawake wa Nairobi hatutaki siasa za ukabila,” akasema Bi Wairimu.
Kwao, mbunge huyo amewahudumia wakazi wa Nairobi bila ubaguzi wowote tangu achaguliwe kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
Ombi la kuondolewa kwa Bi Passaris madarakani kwa sasa linatathminiwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) na lina hoja saba ambazo zimeorodheshwa kama sababu ya kuondolewa kwa mwakilishi huyo wa kike.
Iwapo ombi hilo la Wakenya wanne litapitishwa, Bi Passaris atakuwa mbunge wa kwanza kungólewa madarakani chini ya katiba mpya.
Wanne waliowasilisha ombi la kumwonyesha Bi Passaris mlango ni Shakira Wafula, Domnic Omandi, Marvin Mabonga na Cich Soet.
Wamemshutumu mbunge huyo kwa kukiuka katiba, kudharau maandamano ya amani na ushirikishaji wa umma kwenye miradi ya serikali.
Pia wanadai Bi Passaris amekuwa akiunga dhuluma za polisi dhidi ya waandamanaji na amekosa kumakinikia wajibu wake wa kuwakilisha wanawake wa Kaunti ya Nairobi.
Viongozi hao pia waliunga mkono utawala wa Kenya Kwanza akisema vijana katika Kaunti ya Nairobi wameajiriwa kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na miradi mingine ya serikali.
“Upinzani unafaa kumpa Rais muda wa kufanya kazi tunaposubiri kura ya 2027. Rais amewaajiri vijana na wanafanya kazi kwenye mradi wa nyumba na pia Bima ya Mamlaka ya Kijamii (SHA) pia inafanya kazi. Serikali inafanya kazi na watu wanaiona.”
Mary Wairimu kutoka Dagoretti Kusini alisema kuwa rais aliupata uchumi ambao umesambaratika lakini akaubadilisha na sasa nchi iko dhabiti kifedha.
“Tunaelewa kuwa Roma haikujengwa siku moja. Anafanya kazi kwa hatua na mwisho wa miaka mitano sote tutajionea matunda ya utendakazi wake. Tunasema rais anastahili kuhudumu kwa mihula miwili,” akasema Bi Wairimu.