Kalonzo aishambulia serikali kwa kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari
Makamu huyo wa zamani wa rais ameitaja hatua hiyo kuwa ya kukandamiza, akisema ni dharau kwa Katiba na njama ya utawala wa Kenya Kwanza kuhujumu uhuru wa vyombo vya habari.
Akizungumza akiwa mjini Kisii mnamo Ijumaa alipohitimisha ziara yake ya siku tatu katika eneo la Nyanza Kusini, Bw Musyoka alivitaka vyombo vya habari kuendelea kuangazia maovu yote ya serikali ili iwajibike ipasavyo.
“Tumeona juhudi za makusudi zinazolenga kunyamazisha vyombo huru vya habari katika nchi hii. Wanasema wanataka kurekebisha NMG, Standard Group na Royal Media. Wanawatisha. Tunasema kama Muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kwamba tunasimama na vyombo vya habari huru. Kwamba huwezi kupata nafasi ya kupatiwa matangazo ya kibiashara kutoka kwa serikali. Hii inafanya tuamini kule wanakoelekeza kuna vile wanajuana,” Bw Musyoka alisema akiwa Kisii kabla ya kuondoka kuenda Migori.
Bw Musyoka aliviomba vyombo vya habari kusimama imara na kubaki na kuzingatia malengo yao katika utangazaji wake wote. Alisema Azimio itamkosoa Rais William Ruto kila mara serikali yake itakapochukua uamuzi ambao si sahihi kwa nchi.
Matamshi ya Bw Musyoka yanajiri siku chache tu baada ya wanahabari kutishia kuishtaki serikali ikiwa haitabatilisha uamuzi huo wa kibaguzi.
Hapo awali Katibu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT) Edward Kisiang’ani aliwataka maafisa wa serikali kuzingatia kanuni mpya ya kupeleka matangazo kwa The Star. Chini ya kanuni hizo mpya, Wizara, Idara na Mashirika yote ya serikali ya kitaifa pamoja na Tume Huru na Vyuo Vikuu vya Umma viliagizwa kutangaza kupitia shirika la utangazaji linalomilikiwa na serikali (KBC) na kwenye uchapishaji wa My-Gov, ambao sasa unasambazwa na gazeti moja.
Wakati wote wa ziara yao katika kaunti za Kisii, Nyamira na Migori, Bw Musyoka na na mwenzake wa Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa, wakiandamana na wabunge kadhaa, walikosoa utawala wa sasa kwa ushuru wa juu ambao umewahangaisha Wakenya.
Bw Musyoka alisema tangu Rais William Ruto aingie mamlakani, maisha yamekuwa magumu kwa Wakenya wengi.
Alisema serikali haitaki kuwalipa madaktari lakini inakusanya zaidi ya kutosha kutoka kwa ushuru wa juu ikiwa ni pamoja na tozo ya nyumba ya bei nafuu, ambayo ilirejesha makato ya asilimia 1.5 ya mapato.
“Madaktari hao wamegoma kwa takribani zaidi ya wiki moja sasa. Wamelemaza huduma huku wakisimama kidete na wenzao ambao hawajaajiriwa kazi licha ya kuhitimu baada ya masomo ya miaka mingi. Badala ya Rais kuwasilisha pesa zao, anazitumia kuongeza mgao katika afisi yake na huku mgomo wa matabibu hao ukiwa ni kelele tu,” Bw Musyoka alisema.
Kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa alisema hakuna jinsi serikali ingesema haina pesa za kuheshimu Mkataba wa Makubaliano ya pamoja baina yake na madaktari (CBA) ilhali Rais yuko tayari kutenga pesa za kuwatunuku marafiki ambao walibwagwa chaguzini nafasi za unaibu waziri (CASs).
Aliongeza, “Huwezi kuendelea kuwabebesha Wakenya ushuru wa adhabu mchana na usiku. Umeongeza VAT maradufu kwa bidhaa za kimsingi. Sasa unalenga ushuru wa mkate na maziwa. Sasa ni wakati wa kusema imetosha.”
Bw Musyoka, ambaye alifungua afisi za chama chake katika kaunti za Kisii na Nyamira, aliwataka wafuasi wake kujisajili kuwa wanachama.
Huku kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga akitangaza mipango ya kuwania Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Bw Kalonzo na Bw Wamalwa wamekuwa wakitangatanga nchi nzima ili kujiweka mbele zaidi kuijaza nafasi itakayoachwa na kigogo huyo.
Katika mji wa Rongo, Bw Kalonzo alisimulia jinsi alivyotembea na Bw Odinga kwa miaka mingi. Aliwahakikishia kuwa hata kama Odinga hatakuwepo, Azimio itaendelea kuwa na umoja.