Kalonzo asema hatahudhuria hafla ya Jubilee ya kumtawaza Matiang’i
MUUNGANO wa upinzani unaonekana kuingia katika kipindi kigumu kisiasa baada ya Kiongozi wa chama cha Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, kutangaza kwamba hatahudhuria Mkutano Maalum wa Wajumbe wa Chama cha Jubilee unaotarajiwa kufanyika Ijumaa.
Hafla hiyo inatarajiwa kuthibitisha Bw Fred Matiang’i kama mgombea urais wa chama hicho kwa baraka za Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.
Bw Kalonzo alieleza kuwa sababu ya kutohudhuria ni kutopokea mwaliko rasmi pamoja na masuala nyeti ya kisheria.
“Wakati wa mwisho tulipohudhuria mkutano kama huu, watu walienda mahakamani wakidai kuwa wageni walihusika katika masuala ya ndani ya chama. Kwa hivyo, sitahudhuria,” alisema akiwa katika makao makuu ya chama cha Wiper alipokuwa akikabidhi vyeti vya uteuzi kwa wagombeaji wa chaguzi ndogo zijazo.
Katika hotuba hiyo, Bw Kalonzo pia alikanusha vikali uvumi kuwa anapanga kujiunga na serikali ya Rais William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.
“Huo ni upuuzi mtupu. Waache waseme watakavyo. Mimi nimesalia kuwa mshirika mwaminifu wa muungano wa upinzani na msimamo wetu unabaki kuwa Rais Ruto, kama alivyo Rais wa Malawi Lazarus Chakwera, atakuwa wa muhula mmoja tu,” aliongeza.
Ingawa sababu alizotoa zinaonekana kuwa za kiutaratibu, ukweli ulio wazi ni kuwa muungano wa upinzani unakumbwa na mvutano mkali kuhusu nani atakuwa mgombea wao wa urais mwaka wa 2027. Hii inatishia mshikamano wa muungano huo.
Kwa wiki kadhaa sasa, Bw Fred Matiang’i ameonyesha kwa kauli na vitendo kuwa yuko tayari kuwania urais. Jumanne iliyopita, aliongoza mkutano wa viongozi wa chama cha Jubilee katika Hoteli ya Safari Park, mkutano uliohudhuriwa na Katibu Mkuu Jeremiah Kioni na wabunge wa zamani.
Tukio hilo limechukuliwa kama ushahidi kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta ameamua kumkabidhi uongozi wa chama hicho waziri wake wa zamani wa usalama wa ndani.
Kwa mujibu wa chama cha Jubilee, Bw Matiang’i anachukuliwa kama “kiongozi bora wa mageuzi” atakayeweza kumpinga Rais Ruto, huku Bw Kioni akisisitiza kuwa Matiang’i ana uwezo wa kitaifa na sifa za utawala bora.
Mkutano wa wajumbe wa chama hicho unatarajiwa kuidhinisha mabadiliko makubwa ya uongozi, ukiwemo uwezekano wa Matiang’i kuwa mgombea rasmi wa urais.
Kutohudhuria kwa Bw Kalonzo mkutano huo kunaonyesha kuwa hataki kuhalalisha kwa njia yoyote uongozi wa Matiang’i kama mgombeaji wa urais, kwani hatua hiyo itatafsiriwa kama kumkubali kuwa kifua mbele katika muungano.
Wafuasi wake wanasema amevumilia kwa muda mrefu na sasa ni zamu yake kupeperusha bendera ya upinzani. Wanaamini Matiang’i bado ni kijana na ana muda wa kusubiri uungwaji mkono siku za usoni.
Kwa upande mwingine, wafuasi wa Matiang’i wanasema kuwa kutokana na uzoefu wake serikalini na heshima aliyo nayo kitaifa, yeye ndiye chaguo sahihi linaloleta kizazi kipya na kuachana na historia ya kushindwa kwa upinzani.
Muungano wa upinzani unajumuisha vyama kadhaa: Wiper, Jubilee, PLP (cha Martha Karua), DAP-K (cha Eugene Wamalwa), Democratic Party (cha Justin Muturi), na Democracy for Citizens Party (cha Rigathi Gachagua).
Kalonzo alithibitisha kuwa atahudhuria mkutano wa wajumbe wa chama cha PLP utakaofanyika mwezi ujao.
Bw Gachagua, ambaye aling’olewa kamaNaibu Rais mwaka jana, amemshauri Matiang’i asitumie chama cha Jubilee, bali aunde chama chake ili kujinadi kwa wapiga kura.
Anasema viongozi wanaoweza kujadiliana kwa nguvu ndani ya muungano ni wale walio na msingi wa kisiasa maeneo wanakotoka. Hii ni mojawapo ya mikakati yake ya kulinda kura za Mlima Kenya kuzitumia kwa mazungumzo.
Jubilee, kwa upande wake, inamsawiri Matiang’i kama kiongozi wa kitaifa, si wa kikanda.