• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Kalonzo astaafu siasa Raila akielekea AUC – Wanjigi

Kalonzo astaafu siasa Raila akielekea AUC – Wanjigi

NA JUSTUS OCHIENG

MWANASIASA na mfanyabiashara Jimi Wanjigi amedai kuwa azma ya kiongozi wa Azimio la Umoja, Raila Odinga kuwa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ni hatua ya kujiondoa katika jukwaa la siasa nchini Kenya.

Bw Wanjigi pia alisema kuwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka pia anafaa kustaafu siasa.Katika tamko ambalo huenda likamuudhi Bw Musyoka na kumkasirisha Rais William Ruto, Bw Wanjigi anasisitiza kuwa Bw Musyoka anafaa kuondoka katika siasa na kuwalea wanasiasa vijana, akidai kuwa yeye pia ni miongoni mwa wanasiasa walio na umri mkubwa.

“Kalonzo akome kutupotezea wakati. Yeye ni kati ya wanasiasa wa zamani. Kalonzo hana jipya la kuwapa Wakenya. Tuna tatizo moja humu nchini ambalo ni William Ruto, wala Kalonzo hawezi kumuondoa Ruto na hata kama anaweza kufanya hivyo, hawezi kutatua matatizo ambayo Ruto anasababisha kama kudorora kwa uchumi,”akasema Bw Wanjigi kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali.

Alisema anachopaswa kufanya Bw Musyoka ni kuandaa warithi wake kisiasa katika ngome yake ya Ukambani.

“Anafaa kumfuata Raila tu, na kustaafu kwa heshima. Ikiwa anaamini yeye ni Msemaji wa Wakamba anapaswa kuandaa kizazi kipya ambacho kinafaa katika enzi hii mpya ya siasa.Nadhani amekuwa katika siasa za uchaguzi nchini kwa karibu miaka 40. Ataleta kitu gani kipya? Kweli aache kutupotezea muda na kustaafu,” akasema.

Alitaja hatua ya Raila ya kugombea uenyekiti wa AUC kama wa kijasiri ambalo linafaa kuungwa na serikali bila masharti.

Bw Wanjigi alisema waziri mkuu huyo wa zamani ataachia viongozi wa upinzani viatu vikubwa wanavyopaswa kujaza iwapo azima yake katika AUC itafaulu.

 

  • Tags

You can share this post!

Charlene Ruto: Nataka mume atakayenisaidia kuhudumia vijana

Malimwengu jamaa akiacha mkewe kitandani na kwenda kufanya...

T L