Kalonzo, Ngilu wasusia sherehe ya Mashujaa Dei nyumbani kwao Kitui
KINARA wa Wiper Patriotic Front Kalonzo Musyoka na kigogo wa siasa za Ukambani Charity Ngilu, jana walikosa Sherehe za Mashujaa ambazo ziliandaliwa katika kaunti ya nyumbani ya Kitui.
Rais William Ruto aliongoza taifa kwenye sherehe hiyo katika uwanja wa Ithookwe, mjini Kitui.
Bw Musyoka ambaye ni kinara wa Wiper ndiye kiongozi mwenye ushawishi na usemi mkubwa katika siasa za eneo zima la Ukambani.
Licha ya kutengewa kiti na hata kualikwa rasmi kwa sherehe hiyo, Bw Musyoka hakuonekana Kitui huku wandani wake nao pia wakikosa sherehe hiyo.
Bw Musyoka alihudhuria mazishi ya Raila Odinga katika eneobunge la Bondo Jumapili ambako alimsifu kiongozi huyo kutokana na ushirikiano wa kisiasa wawili hao walikuwa nao 2013, 2017 na 2022 wawili hao wakikosa urais.
Bi Ngilu naye alionekana Alhamisi uwanja wa ndege wa JKIA wakati wa kupokea mwili wa Raila. Pia alihudhuria ibada ya mazishi ya Raila Jumapili na pia ibada ya kumuenzi katika uwanja wa Nyayo.
Tangu Raila ashindwe mnamo 2022, Bi Ngilu hajakuwa akionekana akishiriki hafla ya umma.
Bw Musyoka yupo kwenye ushirikiano wa kisiasa na vinara wengine wa upinzani ambao wamekuwa wakirindima ngoma ya ‘Wan Tam’.
Akiwa Ukambani, Rais alisema kuwa mauti ya Raila yalisababisha aahirishe ziara yake eneo hilo na akaahidi kurejea baada ya siku 12.