Kalonzo: Nilishinikiza Kibaki kumteua Kenyatta kama Naibu Waziri Mkuu
NA WANDERI KAMAU
KIONGOZI wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, amesema kuwa ndiye alimshinikiza Rais Mstafu Mwai Kibaki kuteua Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kama Naibu Waziri Mkuu kwenye baraza la mawaziri baada ya uchaguzi tata wa 2007.
Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni mnamo Jumapili, Machi 10, 2024, Bw Musyoka alisema kuwa kutokana na ghasia za kikabila zilizotokea kati ya 2007/2008, Bw Kibaki hakutaka kumteua Bw Kenyatta ili kutoonekana kama mkabila.
Bw Musyoka alihudumu kama Makamu wa Rais kati ya 2008 na 2013, kwenye Serikali ya Muungano iliyobuniwa baina ya Bw Kibaki na kiongozi wa Azimio, Bw Raila Odinga, ambaye wakati huo alikuwa akiongoza chama cha ODM (hadi sasa).
Serikali hiyo ilibuniwa kufuatia mazungumzo yaliyofanyika kati ya mrengo wa Party of National Unity (PNU) ulioongozwa na Bw Kibaki, huku ule wa ODM ukiongozwa na Bw Odinga.
“Bw Kibaki hakutaka kamwe kumteua Bw Kenyatta kama Naibu Waziri Mkuu. Aliogopa kufasiriwa kama mkabila, hasa ikizingatiwa ghasia za kikabila bado zilikuwa zikiendelea katika baadhi ya sehemu nchini. Alihofia kuelekezewa lawama hizo na washindani wake. Hata hivyo, nilimwambia amteue Bw Kenyatta, kwani Raila alikuwa ashamteua Bw Mudavadi kama Naibu Waziri Mkuu,” akasema Bw Musyoka.
Kufuatia Muafaka wa Makubaliano baina ya Bw Kibaki na Bw Odinga, wawili hao waliwateua Bw Kenyatta na Bw Mudavadi mtawalia kuwa manaibu Waziri Mkuu.
Bw Odinga ndiye aliteuliwa kama Waziri Mkuu, kutokana na mazungumzo yaliyoendeshwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa (UN), marehemu Koffi Annan.
Wakati huo huo, Bw Musyoka amefichua kwamba hatafuti kazi katika serikali ya Rais William Ruto, ila ataendelea kutekeleza majukumu ya kufuatilia utendakazi wa serikali akiwa katika Upinzani.
Pia, amesema kuwa hakuna handisheki yoyote iliyopo baina ya Rais Ruto na Bw Odinga, kufuatia kuwasilishwa kwa Ripoti ya Kamati ya Mazungumzo ya Kitaifa (NADCO).